Boroujerdi: Marekani inaendelea kuwaunga mkono magaidi Syria
Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa ya Siasa za Kigeni ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, vitendo vya Marekani zinaonesha kuwa Washington ingali inaunga mkono ugaidi na vitendo vya kuvuruga amani na utulivu pamoja na kutaka kuzigawa vipande vipande nchi za eneo hili ikiwemo Syria.
Alaeddin Boroujerdi amesema hayo leo pambizoni mwa kikao cha wazi wa Bunge la Iran na kuwaambia waandishi wa habari kwamba kuigawa vipande vipande Syria ni moja ya njama kubwa za Marekani.
Amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuunga mkono umoja wa ardhi yote ya Syria kama ambavyo huko nyuma pia ilikuwa ni moja ya waungaji mkono wakuu wa wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu.
Hati iliyovuja inayojulikana kwa jina la "Washington" ambayo inajumuisha njama za pamoja za Marekani, Uingereza, Ufaransa, Saudia na Jordan inaeleza wazi mpango wa madola hayo wa kuingilia masuala ya ndani ya Syria, kupunguza uwezo wa Rais wa nchi hiyo, kuipokonya serikali uwezo wake wa kusimamia mambo yote ya nchi na kufanya njama za kuudhibiti moja kwa moja Umoja wa Mataifa.
Mkuu huyo wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa ya Bunge la Iran amesisitiza kuwa, hivi sasa suala la kulaani vitendo na siasa za ndani na za kieneo za rais wa Marekani, Donald Trump limetoka katika mkondo wake kwani Washington hivi sasa imeamua kuipaka matope Iran kupitia kufanya mambo ambayo yanaufurahisha utawala wa Kizayuni wa Israel.
Amezungumzia pia mashambulizi ya Uturuki nchini Syria na kusema kuwa, hatua hiyo ya Ankara ni majibu ya vitendo vya Marekani kwani baada ya kushindwa njama za Wamarekani za kuwatumia magaidi wa Daesh, sasa wameamua kuliunga mkono jeshi la Kikurdi la watu 30 elfu kuendeleza njama zake za kuigawa vipande vipande Syria.
Mashambulizi ya kijeshi ya Uturuki katika mji wa Afrin nchini Syria yanayojulikana kwa jina la "Tawi la Mzaituni" yalianza tarehe 20 mwezi huu wa Januari 2018 na yanaendelea hadi hivi sasa.