Ayatullah Nouri-Hamedani: Waislamu wasipoungana, Palestina itatenganishwa na Ulimwengu wa Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i40513-ayatullah_nouri_hamedani_waislamu_wasipoungana_palestina_itatenganishwa_na_ulimwengu_wa_kiislamu
Ayatullah Hussein Nouri Hamedani, mmoja wa Marjaa Taqlidi aliyeko mjini Qom amesisitizia ulazima wa kupatikana umoja baina ya Waislamu duniani na kubainisha kwamba ikiwa Waislamu hawatoungana, maadui wataitenganisha Palestina na Ulimwengu wa Kiislamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 17, 2018 23:43 UTC
  • Ayatullah Nouri-Hamedani: Waislamu wasipoungana, Palestina itatenganishwa na Ulimwengu wa Kiislamu

Ayatullah Hussein Nouri Hamedani, mmoja wa Marjaa Taqlidi aliyeko mjini Qom amesisitizia ulazima wa kupatikana umoja baina ya Waislamu duniani na kubainisha kwamba ikiwa Waislamu hawatoungana, maadui wataitenganisha Palestina na Ulimwengu wa Kiislamu.

Ayatullah Nouri-Hamedani amesema umoja baina ya Waislamu ni amri ya dini na jambo ambalo Iran inatamani lifikiwe na kuongeza kwamba kwa kuungana Ulimwengu wa Kiislamu itawezekana kusimama imara kukabiliana na madhalimu na kuwasaidia wanaodhulumiwa.

Kiongozi huyo wa juu wa kidini amekosoa hatua ya baadhi ya wanasiasa na viongozi wa nchi za Kiislamu ya kupendelea kuwa karibu na Marekani, Uingereza na Wazayuni na kuziusia nchi za Kiislamu kufuata kigezo cha Mapinduzi ya Kiislamu na mwamko wa wananchi wa Iran katika kukabiliana na Uistikbari na Udikteta.

Ayatullah Nouri-Hamedani amesema Jamhuri ya Kiislamu ndio utawala duniani unaotokana zaidi na ridhaa ya wananchi na kufafanua kuwa: hakuna utawala wowote unaopata msukumo wa wananchi kama ulivyo utawala wa Iran na ndiyo sababu ya kuwa na nguvu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo na duniani kwa ujumla.

Ayatullah Nouri-Hamedani ameashiria hali ilivyo katika nchi mbalimbali za Kiislamu ikiwemo Bahrain, Iraq, Afghanistan, Syria na Yemen na kueleza kwamba: Sasa ni wakati wa Waislamu duniani kuungana na kuwa na umoja ili kuweza kupata ushindi dhidi ya maadui wa Uislamu.../