Rouhani: Marekani imekuwa ikivuruga utekelezwaji mapatano ya nyuklia
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Iran inafungamana na ahadi zake katika mapatano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji, JCPOA,' lakini la kusikitisha ni kuwa Marekani daima imekuwa ikiweka vizingiti katika utekelezwaji wa mapatano haya ya kimataifa."
Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo Jumapili katika mazungumzo ya simu na Rais Emanuel Macron wa Ufaransa ambapo amesisitiza kwa mara nyingine kuhusu udharura wa pande zote zilizoafiki mapatano ya JCPOA kufungamana nayo. Rais Rouhani amesisitiza kuwa maadamu upande wa pili unatekeleza mapatano ya JCPOA, Iran nayo itafungamana na mapatano hayo.
Rais Rouhani ameashiria tetesi kuhusu kile ambacho baadhi wanakitaja kuwa ni mazungumzo kamili ya JCPOA na kusema: "Nchi saba zimefikia mapatano na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeyaidhinisha na kwa msingi huo Iran inafungamana kikamilifu na mapatano hayo.
Rais wa Iran amesema ushirikiano wa Iran na Ulaya katika masuala ya kieneo ni mzuri na kuongeza kuwa nchi za Ulaya zinapaswa kuishurutisha Marekani ifungamane na mapatano ya nyuklia.
Rais Rouhani pia ameashiria kuenea njaa na maradhi nchini Yemen sambamba na kuendelea kuhujumiwa nchi hiyo isiyo na ulinzi kusema nchi za Ulaya zinapaswa kuchukua hatua imara kuwasaidia watu madhulumu wa Yemen. Rais wa Ufaransa kwa upande wake amesema nchi yake inataka kuwa na uhusiano imara na Iran. Ameongeza kuwa,Paris itafanya kila iwezalo kulinda mapatano ya JCPOA. Aidha amesisitiza kuwa Ufaransa haitaki mazungumzo mapya kuhusu JCPOA lakini inataka kufanya mazungumzo na Iran kuhusu masuala mengine.
Ikumbukwe kuwa Iran na kundi la nchi za 5+1 ambazo ni Russia, China, Ufaransa, Uingereza, Marekani na Ujerumani ziliafikiana kuhusu mapatano ya nyuklia Julai 2015 baada ya miaka miwili na nusu ya mazungumzo ya kina ya nyuklia. Marekani imekuwa ikivuruga mapatano hayo na kuzuia utekelezwaji wake.