Iran kufuatilia jinai za Israel katika taasisi za kimataifa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i42624-iran_kufuatilia_jinai_za_israel_katika_taasisi_za_kimataifa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesisitza kuwa Iran itaendelea kuunga mkono harakati za mapambano ya kupigania ukombozi wa Palestina kutoka katika makucha ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Apr 04, 2018 02:42 UTC
  • Iran kufuatilia jinai za Israel katika taasisi za kimataifa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesisitza kuwa Iran itaendelea kuunga mkono harakati za mapambano ya kupigania ukombozi wa Palestina kutoka katika makucha ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Aidha amesema Iran itatumia vyombo vya kimataifa, ukiwemo Umoja wa Mataifa, kuwasilisha malalamiko kuhusu jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina.

Zarif ameyasema hayo Jumatano katika mazungumzo ya simu na Ismail Haniya, Mkuu wa Idara ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, ambapo amebainisha kufungamana Iran na taifa la Palestina kufuatia hatua ya wanajeshi wa Israel kuwaua kwa umati Wapalestina 18 waliokuwa wakiandamana kwa amani Ijumaa katika 'Siku ya Ardhi'.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuna haja ya Umoja wa Mataifa na nchi za Kiislamu kuchukua hatua

imara za kuwaunga mkono Wapalestina na kulaani jinai za Israel.

Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wakiwafyatulia risasi Wapalestina waliokuwa wakiandamana kwa amani

Zarif amesema Iran itafuatilia jinai za hivi karibuni za Israel dhidi ya Wapalestina katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote, NAM, na Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu, OIC.

Kwa upande wake, Haniya ameishukuru kwa dhati Iran kutokana na msimamo wake wa kuendelea kuunga mkono harakati ya ukombozi wa Palestina.

Itakumbukwa kuwa siku ya Ijumaa wanajeshi wa utawala wa Israel waliwafyatulia risasi na kuwaua shahidi Wapalestina 18 na kujeruhi mamia ya wengine wakati wa maandamano ya amani ya kutetea haki ya wakimbizi Wapalestina kurejea katika ardhi zao zilizoporwa na kukaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.