Rouhani: Mashambulizi ya Marekani dhidi ya Syria ni uungaji mkono wa ugaidi
(last modified Sat, 14 Apr 2018 17:27:03 GMT )
Apr 14, 2018 17:27 UTC
  • Rouhani: Mashambulizi ya Marekani dhidi ya Syria ni uungaji mkono wa ugaidi

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa mashambulizi yaliyofanywa na Marekani, Uingereza na Ufaransa dhidi ya Iran ni hatua iliyochukuliwa kuimarisha ugaidi katika eneo la Mashariki ya Kati.

Rais Hassan Rouhani amesema katika mazungumzo yake ya simu na Rais Bashar Assad wa Syria kwamba, Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuwa pamoja na serikali na taifa la Syria na kuongeza kuwa: Wakati huu ambapo magaidi wanapata vipigo siku baada ya nyingine, hapana shaka kuwa mashambulizi ya Marekani na washirika wake dhidi ya ardhi ya Syria yana maana ya kuyaunga mkono na kuyahami makundi yaliyoshindwa ya kigaidi. 

Rais Rouhani amesisitiza udharura wa kulindwa ardhi yote ya Syria na kutofanyiwa mabadiliko ya aina yoyote mipaka ya kijografia ya nchi hiyo na kusema: Kuwepo majeshi ya kigeni huko Syria bila ya ruhusa ya serikali ya Damascus ni kinyume cha sheria za kimataifa na uvamizi dhidi ya nchi hiyo. 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, hakuna nchi yoyote ya kigeni inayoweza kuchukua maamuzi kuhusu mustakbali wa Syria, na mchukuaji maamuzi pekee katika suala hilo na wananchi wa Syria wenyewe. Amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuwa pamoja na serikali na taifa la Syria.

Rais Hassan Rouhani

Kwa upande wake Rais Bashar Assad wa Syria ameupongeza Umma wa Kiislamu kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya leo (tarehe 27 Rajab) ya kukumbuka tukio la kupewa Utume na kubaathiwa Nabii Muhammad (saw) na kusema: Mashambulizi yaliyofanywa na Marekani na waitifaki wake dhidi ya Syria hayatateteresha azma kubwa ya taifa na serikali ya nchi hiyo ya kudumisha njia ya mapambano.

Rais wa Jamhuri ya Syria amelishukuruu taifa na serikali ya Iran kutokana na himaya na misaada yake kwa taifa na serikali ya Syria na kusema: Baada ya kushindwa kufikia malengo yao kupitia njia za kisiasa, Marekani na waitifaki wake wameamua kukanyaga sheria za kimataifa na kuishambulia Syria.