Iran yasema uwezo wake wa makombora ni kwa ajili ya kujilinda
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i46617-iran_yasema_uwezo_wake_wa_makombora_ni_kwa_ajili_ya_kujilinda
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa hatua ya Iran ya kuimarisha uwezo wake wa makombora ni kwa ajili ya kujihami.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 07, 2018 07:38 UTC
  • Iran yasema uwezo wake wa makombora ni kwa ajili ya kujilinda

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa hatua ya Iran ya kuimarisha uwezo wake wa makombora ni kwa ajili ya kujihami.

Bahram Qassemi ameyasema hayo ikiwa ni radiamali kwa madai ya kujikariri yaliyotolewa jana Ijumaa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian katika mahojiano na Radio RTL, kwamba mradi wa makombora wa Iran hauna malengo ya kujilinda.

Qassemi amebainisha kuwa, "Madai kama hayo dhidi ya Iran hayana msingi wowote na yanatokana na baadhi ya watu kutokuwa na taarifa sahihi kuhusiana na hali halisi ya hivi sasa katika eneo la Mashariki ya Kati."

Amefafanunua kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa mstari wa mbele katika jitihada za kuimarisha usalama, uthabiti na amani katika eneo hili, na kwamba mradi wa makombora wa Tehran haulengi kuihujumu nchi yoyote, bali kujihami. 

Sehemu ndogo ya makombora ya balestiki ya Iran

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kwamba uwezo wake wa kiulinzi, makombora na zana nyingine za kiulinzi ni wa hapa hapa nchini na kwamba unalenga kuzuia mashambulizi tarajiwa ya maadui.

Tehran imekuwa ikisisitiza kwamba, kamwe haitasalimu amri mbele ya mashinikizo ya adui kuhusiana na uwezo huo wa kiulinzi bali itaendelea kuuimarisha zaidi.