AEOI: Iran ipo tayari kuimarisha urutubishaji urani JCPOA ikifeli
Behrouz Kamalvandi, Msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (AEOI) amesema Tehran iko tayari kuimarisha urutubishaji urani kwa kiwango cha juu iwapo jitihada za Umoja wa Ulaya za kuyanasuru makubaliano ya nyuklia ya Iran zitagonga mwamba.
Amesema "Bila shaka kwa sasa tunaendelea kutekeleza wajibu wetu wa kufungamana na makubaliano hayo yanayofahamika kama JCPOA, lakini wakati huo huo tunatathmini kwa kina senario zote iwapo mazungumzo na nchi za Ulaya hayatazaa matunda. Tumejiandaa."
Afisa huyo wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amekariri kuwa, Tehran imeufahamisha Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kuwa imeanzisha mchakato wa kuimarisha uwezo unaohitajika wa kuzalisha gesi aina ya UF6 na UF4 na ujenzi wa kiwanda cha kutengenza mashinepewa (centrifuge), mambo yanayohitajika kwa ajili ya kurutubisha madini ya urani, yanayotumika katika uzalishaji wa nishati ya nyuklia.
Hivi karibuni Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei alitoa amri kwa Shirika la Atomiki la Iran na kusema: "Matayarisho yanayohitajika kwa ajili ya kufikiwa kiwango cha SWU 190,000 yaanze kutekelezwa haraka katika fremu ya mapatano ya JCPOA."
Mnamo Mei 8, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa nchi yake imeondoka katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, ambayo yalifikiwa baina ya Iran na madola sita makubwa duniani, yaani China, Russia, Uingereza, Ufaransa, Marekani pamoja na Ujerumani mwaka 2015.
Rais wa Marekani pia alitangaza kurejesha tena vikwazo dhidi ya Iran, jambo ambalo limekosolewa vikali kimataifa. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeishtaki Marekani katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu ICJ, kufuatia hatua hiyo ya Washington iliyo kinyume cha sheria ya kuiwekea tena Tehran vikwazo vya upande mmoja kuanzia mwezi ujao wa Agosti.