Larijani: Adui hawezi kuzungumza na Iran kwa kutumia lugha ya mabavu
Spika wa Bunge la Iran amesema kuwa maendeleo ya utengenezaji wa makombora ya Jamhuri ya Kiislamu ni makubwa kiasi kwamba sasa adui hawezi kuzungumza na Iran kwa kutumia lugha ya vitisho na vita.
Dakta Ali Larijani amesema katika kongamano la mabalozi na wawakilishi wa Iran katika nchi za kigeni kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ina uwezo mkubwa katika masuala ya kiulinzi na uwezo huo unailinda Iran ya Kiislamu.
Spika wa Bunge la Iran amesema kuwa, adui anajua vyema kwamba kutumia lugha ya vitisho na vita dhidi ya Iran hakuna tija wala faida yoyote kwa sababu hiyo hazungumzii suala la makombora ya Iran bali anataka kufanyike mazungumzo kuhusu uwezo na masafara ya makombora hayo.
Larijani pia ameashiria azma kubwa ya Iran ya kupambana na ugaidi huko Iraq na Syria na kusema: Pigo kubwa la Iran dhidi ya magaidi huko Syria na Iraq limeimarisha utulivu na amani nchini Iran.
Vilevile Spika wa Bunge la Iran ameitaja hatua ya hivi karibuni ya Bunge la Israel ya kupasisha sheria ya kibaguzi inayoitambua Israel kuwa ni dola la Mayahudi pekee kuwa ni kucheza na moto katika eneo la Mashariki ya Kati na kuongeza kuwa: Israel imetumia udhaifu wa baadhi ya tawala za eneo hilo kwa ajili ya kuyasaidia makundi ya kigaidi.