Abdollahian: Kukombolewa miinuko ya Golan ya Syria ni jambo linalowezekana
Mshauri maalumu wa Spika wa bunge la Iran katika masuala ya kimataifa amesema: kukombolewa miinuko ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu kunawezekana kwa juhudi za wananchi wa Syria.
Katika ujumbe aliotuma kupitia ukurasa wake wa Twitter wa kuwapongeza wananchi wa Syria, vikosi vya ulinzi na rais wa nchi hiyo kwa kukombolewa mji wa Quneitra kutoka kwenye makucha ya magaidi wa genge la Jabhatu-Nusra na Wazayuni, Hossein Amir-Abdollahian, ameandika: ushindi huu unamaanisha kuwa kukombolewa miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu, nako pia kunaweza kuthibiti kwa juhudi na hima ya jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Syria.
Siku ya Alkhamisi ya tarehe 26 Julai, jeshi na vikosi vya wananchi wa Syria vilipandisha na kupeperusha bendera ya nchi hiyo karibu na kivuko cha Quneitra katika eneo la Golan baada ya kuukomboa mji huo kutoka kwenye makucha ya magaidi na wazayuni.
Miinuko ya Golan ni sehemu ya ardhi ya Syria, lakini mwaka 1967 utawala haramu na ghasibu wa Kizayuni wa Israel ulivamia na kuanza kulikalia kwa mabavu eneo lenye ukubwa wa kilomita 1,200 la ardhi za Golan; na mnamo mwaka 1981 ukaliunganisha eneo hilo na ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.
Jeshi la Syria, hivi sasa limejizatiti kwenye eneo la Quneitra kwa lengo la kuukomboa ukanda wa mpakani wa miinuko ya Golan.../