Oct 15, 2018 14:12 UTC
  • Qassemi: Iran na Afghanistan zina historia kongwe katika uhusiano wa pande mbili

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Afghanistan ni jirani muhimu wa Iran na kwamba, historia kongwe iliyoko katika uhusiano wa pande mbili inalazimu nchi hizo kuwa na ushirikiano zaidi katika nyuga mbalimbali.

Bahram Qassemi amesema hayo  leo hapa mjini Tehran katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari ambapo akijibu swali kuhusiana na uchaguzi ujao wa Bunge nchini Afghanistan uliopangwa kufanyika tarehe 20 mwezi huu ameeleza kuwa, kwa kuzingatia matukio chanya ya usalama nchini Afghanistan hususan katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, ana matumaini uchaguzi huo utafanyika katika anga tulivu.

Qassemi amesema pia kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakaribisha kwa mikono miwili kupanuliwa ushirikiano kati ya Tehran na Kabul katika nyanja mbalimbali.

Rais Hassan Rouhan wa Iran (kulia) na Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan katika moja ya mazungumzo ya viongozi wa ngazi za juu wa Iran na Afghanistan (picha ya maktaba)

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia pia ushiriki wa Iran katika ukarabati wa Syria na kusema kuwa, kwa kuzingatia uwepo wa kiushauri wa Tehran huko Syria kwa ajili ya kupambana na ugaidi, Tehran itashiriki pia katika ukarabati wa nchi hiyo kwa ridhaa na matakwa ya serikali ya Damascus.

Bahram Qassemi amezungumzia pia uingiliaji wa Marekani katika masuala ya Syria na kusema kuwa, Washington inafanya uingiliaji huo bila ya idhini ya serikali ya Damascus hatua ambayo ni kinyume cha sheria na inayokinzana wazi kabisa na kanuni na sheria za kimataifa.

Tags