Kiongozi Muadhamu asisitiza udharura wa kupambana na ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i4927-kiongozi_muadhamu_asisitiza_udharura_wa_kupambana_na_ugaidi
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, madola yanayodai kupambana na ugaidi hususan Marekani hayana nia ya kweli katika uwanja huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 12, 2016 12:23 UTC
  • Kiongozi Muadhamu asisitiza udharura wa kupambana na ugaidi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, madola yanayodai kupambana na ugaidi hususan Marekani hayana nia ya kweli katika uwanja huo.

Ayatullah Ali Khamenei, amesema hayo katika mazungumzo yake na Rais Nursultan Nazarbayev wa Kazakhstan na kusisitiza udharura wa kuzidishwa ushirikiano wa nchi mbili katika nyanja mbalimbali ikiwemo vita dhidi ya ugaidi.

Katika uwanja huo Kiongozi Muadhamu amesema misaada ya Wamarekani kwa kundi la Daesh huko Iraq ni mfano wa wazi wa mienendo ya kindumakuwili na isiyo na kweli ya miungano mbalimbali inayodai kupambana na ugaidi na kusema: Ili kuhalalisha mienendo hiyo, nchi hizo zimeugawa ugaidi katika ugaidi mzuri na ugaidi mbaya.

Ayatullah Khamenei ameashiria uraia wa nchi za Ulaya wa watekelezaji wa mashambulizi ya kigaidi barani Ulaya na vilevile suala la kuwepo raia wengi wa nchi hizo katika makundi ya kigaidi huko Syria na Iraq na kusema kuwa, ukweli huo unathibitisha kwamba, Magharibi hususan na Marekani haina azma na nia ya kweli ya kupambana na ugaidi.

Mienendo ya kindumakuwili katika suala la kupambana na ugaidi imekuwa sababu ya kuenea zaidi hali ya ukosefu wa usalama katika maeneo mbalimbali duniani. Kwa sasa nchi nyingi zinakabiliwa na hatari na tishio hilo la ugaidi ambao hii leo haujui mipaka ya nchi au bara. Inatupasa kuelewa pia kuwa, ugaidi una sababu mbalimbali, na matamshi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mazungumzo yake na Rais wa Kazakhstan yameweka wazi sehemu ndogo tu ya sababu za janga hilo.

Mienendo ya kindumakuwili ya nchi za Magharibi kuhusu ugaidi na kuyatumia makundi ya kigaidi kama Daesh kwa ajili ya kutimiza malengo yao ni miongoni mwa sababu za kushamiri na kueneza zaidi ugaidi katika maeneo mbalimbali duniani.

Pamoja na hayo, suala linalotia wasiwasi zaidi ni kwamba, kwa upande mmoja nchi za Kiislamu hii leo zinakabiliwa na hatari ya makundi ya kigaidi yanayohujumu Uislamu na Waislamu kwa kutumia jina la Uislamu, na katika upande mwingine madola makubwa ya Magharibi hayataki kuona nchi za Waislamu zikishikamana na kuwa pamoja.

Njia ya kupambana na tishio na njama hizo ni kukabiliana na sababu zote zinazopelekea kujitokeza ugaidi na kukausha kabisa mizizi ya makundi yenye misimamo mikali. Hata hivyo ili kufikia lengo hilo kuna ulazima wa kutayarishwa fursa na mazingira mazuri ya ushirikiano. Mtazamo wa Iran kuhusu uhusiano na nchi mbalimbali ikiwemo Kazakshtan, unaweza kutathminiwa katika uwanja huu. Hili ndilo suala lililotiliwa mkazo na kusisitizwa katika mazungumzo ya Rais Nursultan Nazarbayev wa Kazakhstan na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kwamba, migogoro ya kimataifa imefikia kiwango ambacho iwapo hakutakuwepo ushirikiano wa nchi zote basi wanadamu wote watapatwa na madhara ya ugaidi. Ni kwa sababu hii pia ndipo Kiongozi Muadhamu akasisitiza kuwa, njia pekee ya kupambana na ugaidi ni kuwa na irada na azma ya kweli ya kupambana na janga hilo na kujiepusha na mienendo ya kindumakuwili katika uwanja huo.

Suala hilo pia limesisitizwa na Rais Nursultan Nazarbayev wa Kazakhstan ambaye amesema kuhusu umoja wa ulimwengu wa Kiislamu kwamba: Tunapaswa kuionyesha dunia kwamba, Uislamu ni dini ya maendeleo, umoja na kupambana na ugaidi.