Zarif: Marekani inatumia vibaya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i49966-zarif_marekani_inatumia_vibaya_baraza_la_usalama_la_umoja_wa_mataifa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hayaizuii Iran kuzalisha makombora na amekosoa migongano inaoonekana katika matamshi ya maafisa wa serikali ya Marekani kuhusu azimio nambari 2231 la baraza hilo.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Dec 05, 2018 03:04 UTC
  • Zarif: Marekani inatumia vibaya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hayaizuii Iran kuzalisha makombora na amekosoa migongano inaoonekana katika matamshi ya maafisa wa serikali ya Marekani kuhusu azimio nambari 2231 la baraza hilo.

Muhammad Javad Zarif ameyasema hayo baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo kudai kuwa, hivi karibuni Iran ilifanya majaribio ya kombora la balestiki la masafa ya kati ambalo lina uwezo wa kubeba vichwa kadhaa. Madai hayo ya Pompeo ambayo hayakuambatanishwa na ushahidi wa aina yoyote yanasema majaribio hayo yanakinzana na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amejibu madai hayo katika ukurasa wake wa Twitter akisema: Utumiaji mbaya wa Marekani wa Baraza la Usalama la UN hauwezi kuficha makosa ya nchi hiyo ya kutoheshimu majukumu yake ya kimataifa. 

Zarif ameongeza kuwa, maafisa wa serikali ya Marekani wanakiri kwamba, azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama haliwezi kuzuia uwezo wa kujihami wa Iran; hivyo ni vyema badala ya kutaka kudhoofisha azimio hilo, wahakikishe pande zote zinaliheshimu na kulitekeleza.

Donald Trump

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameambatanisha maandishi hayo na matini iliyoandikwa na mjumbe maalumu wa Marekani katika masuala ya Iran, Brian Hook.

Itakumbukwa kuwa, tarehe 20 Septemba mwaka huu wa 2018, Hook alitangaza kuwa, azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaitaka Iran isifanye shughuli zinazohusiana na  makombora ya balestiki yanayoweza kubeba silaha za nyuklia na si vinginevyo.