Rais Rouhani asisitiza kustawishwa uhusiano wa Iran na nchi za Kiafrika
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kustawishwa uhusiano na kuweko ushirikiano wa karibu baina ya Tehran na nchi za Kiafrika zikiwemo Tunisia, Sierra Leone na Mali ni jambo la dharura.
Rais Rouhani alisema hayo jana wakati alipopokea hati za utambulisho za mabalozi wapya wa Tunisia, Mali na Sierra Leone hapa mjini Tehran na kusema kuwa, Iran iko tayari kupanua ushirikiano wake na nchi za Kiafrika katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kielimu, vyuo vikuu na kilimo.
Rais Rouhani amebainisha kuwa, kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu, Iran ilikuwa kituo kikubwa cha Marekani katika Mashariki ya Kati na kuongeza kuwa, katika Mapinduzi ya Kiislamu, wananchi wa Iran waliamua nchi yao isiwe tena kituo cha dola lolote lile kubwa duniani na badala yake iwe kituo cha kutimiza malengo na matukufu yake tu.
Kwa upande wake Alie Badara Kamara, balozi mpya wa Sierra Lieone mjini Tehran amesema kuwa, nchi yake inataka kustawishwa zaidi uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hasa katika nyanja za elimu, vyuo vikuu, sekta ya afya na matibabu.
Balozi mpya wa Mali mjini Tehjran kwa upande wake ameshukuru Iran kwa misaada yake kwa nchi hiyo na kusema kuwa, Tehran na Bamako zina misimamo ya inayofanana katika asasi na jumuiya mbalimbali za kimataifa na kwamba, hilo linaweza kuwa uwanja mzuri wa kuimarishwa zaidi ushirikiano wa nchi mbili hizi katika nyanja mbalimbali.