Rais wa Iran: Wakimbizi Waislamu Warohingya werejeshwe haraka nchini Myanmar
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i52061-rais_wa_iran_wakimbizi_waislamu_warohingya_werejeshwe_haraka_nchini_myanmar
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza udharura wa kuwepo utulivu na amani nchini Myanmar na kusema kuwa wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya wanapaswa kurejeshwa haraka na kwa amani katika makazi yao nchini Myanmar.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 10, 2019 01:18 UTC
  • Rais wa Iran: Wakimbizi Waislamu Warohingya werejeshwe haraka nchini Myanmar

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza udharura wa kuwepo utulivu na amani nchini Myanmar na kusema kuwa wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya wanapaswa kurejeshwa haraka na kwa amani katika makazi yao nchini Myanmar.

Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo jana Jumamosi mjini Tehran wakati alipopokea vitambulisho vya Mukyu Ung, balozi mpya wa Myanmar nchini Iran. Rais Rouhani amesema amani na usalama katika nchi yoyote hupatikana kwa kushirikiana watu wa kaumu na jamii  zot na ameeleza matumaini kuwa: "Jitihada za serikali ya Myanmar zitazaa matunda na amani na usalama utarejea nchini humo ili wakimbizi waweze kurejea katika nchi yao."

Rais Rouhani pia amesema kuna uwezekano wa kuimarishwa uhusiano wa Iran na Myanmar na kuongeza kuwa: "Nchi mbili zinaweza kushirikiana katika nyanja kama vile huduma za uhandisi, uwekezaji, biashara na utalii."

Rais Rouhani wa Iran akipokea vitambulisho vya Mukyu Ung, balozi mpya wa Myanmar mjini Tehran, 03/09/2019

Kwa upande wake, Mukyu Ung, balozi mpya wa Myanmar nchini Iran ameishukuru Iran kwa kuwa na uhusiano mzuri na nchi yake.

Kuhusiana na hali ya Waislamu wa jamii ya Rohingya, Mukyu Ung amesema: "Serikali ya Myanmar inajitahidi kuchukua hatua za kuwarejesha wakimbizi katika maeneo yao na kuna mapatano yaliyofikiwa na Bangladesh pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa."