Kukariri Trump porojo lake katika ujumbe wa Nowruz kwa Wairani
Rais wa Marekani Donald Trump, tangu kwenye kampeni zake za uchaguzi wa rais na mpaka baada ya kuingia Ikulu ya White House Januari 2017, amekuwa akitumia lugha kali na maneno machafu dhidi ya Iran, kwa lengo la kuudhoofisha na kuuangusha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Baada ya kutangaza kujitoa Marekani kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kurejesha tena vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran, Trump alianzisha vita vikali vya kiuchumi, lengo likiwa ni kuzifanya hali za maisha ya wananchi wengi ziwe mbaya ili kuibua malalamiko na machafuko ndani ya Iran. Lakini kwa upande wa kieneo pia, serikali ya Trump ikaamua kutumia kisingizio cha utekelezaji wa hati ya kistratejia ya usalama wa taifa ya Marekani ya mwaka 2017 kuanzisha kampeni na mkakati mkubwa wa kuunda muungano wa kieneo, kwa madhumuni ya kuidhibiti Iran na kuilazimisha ibadilishe sera na hatua zake katika eneo hili la Magharibi ya Asia.

Licha ya muelekeo wa kiuadui na hatua za kihasama alizochukua Trump dhidi ya Wairan, katika ujumbe wake wa Nowruz aliotoa kwa mnasaba wa kuanza mwaka 1398 hijria shamsia, kwa mara nyingine, rais huyo wa Marekani amerudia tena kauli zake za porojo na za kubwabwaja, za kuzusha madai ya uongo na tuhuma kadha wa kadha dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Huku akidai kuonyesha mshikamano na wananchi wa Iran, Trump amedai kuwa, hatonyamaza kimya kuhusiana na matakwa ya wananchi hao. Trump amedai kuwa: Wananchi wa Iran wangali wanashindwa kushiriki kikamilifu katika kufurahia masiku haya. Rais huyo wa Marekani anajifanya kuwa ana uchungu na wananchi wa Iran, huku akiwa ameiwekea nchi hii vikwazo vikubwa na vikali zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia, ili kwa dhana yake aipigishe magoti Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Huku akidai kwamba wananchi wa Iran wanataka kuirejesha tena historia yao ya kujivunia, utamaduni na hadhi yao halisi duniani, Trump amesema: Maisha ya kila siku ya Wairani yanakinzana na tafsiri ya Nowruz, ambayo maana yake ni siku mpya. Rais wa Marekani anadai kuwa, Wairani hawana furaha, akiwa amesahau kwamba vikwazo vya kidhalimu ilivyoweka nchi yake baada ya kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, ambavyo kiutekelezaji, vimejumuisha hata vifaa vya tiba na dawa, ndiyo sababu ya kushadidi mbinyo na mashinikizo dhidi ya Iran. Serikali ya Trump imeziwekea vikwazo hata ndege za Iran kwa kuyazuilia mashirika ya ndege ya Iran yasiuziwe vipuri wala kupatiwa huduma nyingine za lazima, na hivyo kuhatarisha moja kwa moja maisha ya raia wa kawaida wa Iran.

Lakini licha ya yote hayo, kwa kipindi chote hiki cha miaka 40, wananchi wa Iran wamethibitisha kuwa, propaganda na mashinikizo ya Marekani hayawezi kuwaathiri hata chembe na kuwafanya warudi nyuma katika kuuunga mkono mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu; na wala hawako tayari kupoteza uhuru na kujitawala kwao na kuridhia matakwa ya kibabe ya Washington. Lakini pia taifa la Iran limethibitisha kuwa, linao uwezo wa kuvivuka kwa mafanikio vikwazo vya Marekani na kuzishinda siasa za kihasama za Trump. Barbara Slavin, mtaalamu wa masuala ya Iran katika Baraza la Atlantiki mjini Washington anasema: "Hivi sasa jamii ya kimataifa haiko pamoja tena na Marekani. Tuko katika mazingira ambayo, serikali ya Trump inafanya kila njia ili kuilazimisha jamii ya kimataifa ifuate siasa zake, wakati nchi nyingi hazikubaliani na siasa hizo. Kwa hivyo katika awamu ya mwanzo, mfumo wa Iran umeshinda; na karata za turufu ulizopata kutokana na makubaliano ya nyuklia zimezidi kuuimarisha, na hivi sasa katika uga wa kimataifa, nchi hii inatazamwa kama mmoja wa wadau wakuu."

Marekani imekuwa ikidhani kwamba, kwa kutumia vita vya kipropaganda na kuiwekea Iran vikwazo vikali zaidi vya kiuchumi kuwahi kushuhudiwa, itaweza kuipigisha magoti iridhie kutekeleza matakwa yake. Tafsiri halisi ya siasa hizo za Marekani ni kuingilia moja kwa moja masuala ya ndani ya Iran, ambako ni kinyume cha sheria kwa mujibu wa sheria za kimataifa na kunakinza na kanuni za kimataifa na Hati ya Umoja wa Mataifa. Mtazamo na muelekeo wa Trump kuhusiana na Iran unazidi kuthibitisha kuwa, rais huyo wa Marekani hana uelewa wowote kuhusu Wairani. Kwani tajiriba ya miaka 40 iliyopita imeonyesha kuwa, kadiri mashinikizo ya kigeni dhidi ya Iran yanavyoongezeka, ndivyo umoja na mshikamano wa watu wake pia unavyozidi kuwa mkubwa zaidi.../