Kutosalimu amri katu taifa la Iran mbele ya mashinikizo ya Marekani
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa radiamali kwa hatua zilizo dhidi ya Iran za Rais Donald Trump na kusema kuwa, Wairani katu hatawasalimu amri mbele ya mashinikizo ya Marekani.
Dakta Muhammad Javad Zarif alisisitiza Jumapili ya juzi katika ujumbe aliouandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Siasa za Rais Donald Trump mkabala na Iran zimeshindwa na kukonga ukuta. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema kuwa: Trump amekuwa akitumia wenzo wowote uliofeli katika siasa zake mkabala na Iran, na kutaka kuonyesha kuwa eti ni mafanikio.
Katika matamshi yake ya karibuni kabisa, Rais Donald Trump aliandika siku ya Jumamosi katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, kujiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yalikuwa ni mafanikio katika sera za kigeni za Washington. Hatua ya Trump ya kuiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ilikuwa na lengo la kushadidisha mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi dhidi ya taifa la Iran. Hata hivyo, Marekani haijapata mafanikio katika uwanja huo.
Tajiriba ya kihistoria imethibitisha kwamba, taifa la Iran katu haliwezi kusalimu amri mbele ya Marekani kupitia njia ya kuongeza mashinikizo. Faili la kushindwa Marais wa zamani wa Marekani katika uwanja huo, linaweza kuwa darsa na funzo kwa Trump kwamba, Wairani katu si watu wa kusalimu amri kupitia mashinikizo.
Serikali mbalimbali zilizotawala nchini Marekani zilitumia kila wenzo wa mashinikizo katika kipindi cha miaka 40 iliyopita ili kutoa pigo kwa Iran. Hata hivyo natija ya siasa hizo za kibabe na utumiaji mabavu, haikuwa nyingine bighairi ya kupatikana umoja na mshikamano zaidi miongoni mwa wananchi wa Iran na kuifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa na nguvu na uwezo zaidi katika nyuga mbalimbali.
Katika kipindi cha vikwazo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepata mafanikio makubwa katika nyuga za kisiasa, kiuchumi, kijeshi na kiulinzi mambo ambayo yamelifanya taifa hili la Kiislamu kuzidi kuwa lenye taathira na nguvu maradufu kieneo na kimataifa. Kuwa na taathira na ushawishi Iran katika eneo, ni ishara ya wazi ya kuwa na nguvu Iran, na hili ni jambo lililomsukuma Donald Trump aiondoe nchi yake katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ili kwa dhana yake, eti aifanye Tehran isalimu amri na kufuata matakwa ya Washington.
Lakini kinyume na matarajio yake, hatua hiyo imeshadidisha upinzani wa jamii ya kimataifa dhidi ya hatua za upande mmoja za Rais huyo wa Marekani. Fauka ya hayo, hatua hiyo ilmeifanya Marekani iendelee kutengwa kisiasa katika uga wa kimataifa. Hatua ya Trump ya kupuuza makubaliano na sheria za kimataifa na kuiondoa nchi yake katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ili kushadidisha mashinikizo dhidi ya Iran nayo imeifanya serikali ya Washington ikabiliwe na upinzani hata ndani ya Marekani kwenyewe.
Katika uwanja huu, John Kerry, Waziri wa zamani wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani ametahadharisha kuhusiana na siasa za uchupaji mipaka za Donald Trump pamoja na washirika wake dhidi ya Iran. Kituo cha Kifikra cha Marekani cha Brookings kilikiri siku ya Jumamosi kwamba, utendaji wa serikali ya Trump wa kutaka kuifanya Iran isalimu amri mbele ya matakwa ya Marekani umefeli na kugonga mwamba.
Wataalamu wa Kituo cha Kifikra cha Brookings wamesisitiza kuwa: Sababu kuu ya kushindwa stratijia ya serikali ya Donald Trump mkabala na Iran ni kusimama kidete Wairani mbele ya matakwa ya Marekani na kwamba, nchi yao inakabiliwa na ubabe na ubeberu wa Washington.
Historia ya miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni ushahidi tosha kwamba, kila mara Marekani inaposhadidisha vitendo vyake vya ubeberu na utumiaji mabavu dhidi ya Iran, basi ndivyo ambavyo pia kusimama kidete wananchi wa taifa hili kunavyoongezeka na kuushinda mkakati na stratijia ya Marekani. Filihali pia kujiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA na kushadidisha ikulu ya White House mashinikizo yake dhidi ya taifa la Iran, hakutoifanya Washington ifikie malengo yake.
Kwa hakika utendaji na uchukuaji hatua za upande mmoja wa Marekani, hauna madhara kwa nchi maalumu tu, bali hatua hizo zina madhara kimataifa pia, kwani kuweko umoja kwa ajili ya kukabiliana na na aina hii ya utendaji ya Rais Donald Trump ni dharura ya kilimwengu. Trump anaihesabu hatua yake ya kuiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kuwa ni mafanikio, katika hali ambayo, kwa hatua yake hiyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeimarika na kushikamana zaidi huku jamii ya kimataifa nayo, ikijitenga na Marekani.