Apr 21, 2019 13:42 UTC
  • Safari ya Waziri Mkuu wa Pakistan mjini Tehran; ukurasa mpya wa ushirikiano wa pande mbili

Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan leo Jumapili ameanza safari ya siku mbili humu nchini kwa mwaliko rasmi wa Rais Hassan Rouhani wa Iran.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan, kabla ya kuelekea mjini Tehran Imran Khan, ambaye anaongoza ujumbe wa ngazi za juu wa nchi yake, atasimama kwa muda katika mji mtakatifu wa Msh'had (mashariki mwa Iran) kwa ajili ya kuzuru Haram Takatifu ya Imam Ali Ridha (as). Waziri Mkuu huyo wa Pakistan pia anatazamiwa kushiriki kikao cha pamoja cha kibiashara kati ya wafanyabiasha wa Iran na Pakistan. Licha ya kuwa safari hii inaashiria umuhimu wa kibiashara na kiuchumi wa nchi mbili lakini ni wazi kuwa ushirikiano wa viongozi wa nchi mbili hizi katika uwanja wa kupambana na ugaidi na juhudi za kuimarisha usalama katika mpaka wao wa pamoja  ni jambo linalopewa uzito katika safai hii. Ni kutokana na ukweli huo ndipo katika mazungumzo yao ya simu muda mfupi kabla ya kuanza safari hiyo, Muhammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Shah Mahmoud Quraishi waziri mwezake wa mambo ya nje wa Pakistan wakasisitiza umuhimu wa kuimarishwa ushirikiano wa nchi mbili kwa shabaha ya kupambana na ugaidi.

Imran Khana, Waziri Mkuu wa Pakistan azuru Haram ya Imam Ridha (as) mjini Mash'had, Iran

Kuhusu suala hilo Iran na Pakistan zimefikia maelewano ya kijeshi kuhusu jinsi ya kuimarisha ushirikiano wa masuala ya kiusalama kwa madhumuni ya kupambana na ugaidi na kubadilishana habari za kiintelijensia. Safari ya kihistoria iliyofanywa humu nchini miaka miwili iliyopita na Jenerali Qamar Javed Bajwa, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Pakistan, na vilevile safari iliyofanywa hivi karibuni nchini Pakistan na Meja Jenerali Muhammad Baqiri, Kamanda Mkuu wa Majeshi ya Jamuri ya Kiislamu ya Iran ni jambo linalotoa ujumbe maalumu katika uwanja huo. Meja Jenerali Baqiri alisema kuhusu umuhimu wa kulindwa usalama katika eneo la kusini magharibi mwa Asia lwamba: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina jukumu muhimu la kukabiliana na vitisho na inaamini kuwa njia bora ya kuimarisha usalama ni ushirikiano kati ya nchi za eneo na kunufaika na uwezo wa pande mbili.'

Hissam Kian Muqaddam, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema kuhusu ukweli huo kwamba: Tokea wakati wa kutangazwa rasmi safari ya Imran Khan nchini Iran na kufahamika tarehe ya safari hiyo, makundi ya kigaidi yenye misimamo ya kupindukia mipaka na ambayo yanadhaminiwa kifikra na kifedha na Saudi Arabia katika eneo la Balochestan nchini Pakistan yameongeza harakati zao za kigaidi katika eeo hilo. Kwa mtazamo wa mchambuzi huyo wa masuala ya kisiasa, hata kama hatupasi kutarajia zaidi ya hayo kutoka kwa Saudi Arabia ambayo ina rekodi mbaya na ya uhasama dhidi ya Iran, lakini suala hilo ni kengele ya hatari kwa maana kwamba lengo la Saudia ni kuharibu uhusiano wa nchi mbili hizi jirani na kuvuruga usalama na uthabiti wa eneo.

Imran Khan akizungumza na viongozi wa kieneo, mara tu baada ya kuwasili mjini Mash'had

Iran na Pakistan zikiwa nchi mbili jirani za Kiislamu zina mtazamo mmoja kuhusu udharura wa kuimarishwa uhusiano wa pande mbili na ushirikiano kwa ajili ya kutatua migogoro ya kieneo. Uhusiano wa Pakistan na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambazo ni waanzilishi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ECO na Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu OIC unatokana na masuala ya pamoja ya kihistoria, kiutamaduni, kidini na mfungamano imara wa watu wa nchi mbili hizi. Kila mara tukio fulani linapotokea nchini Pakistan watu wa Iran huchukua hatua za haraka kwa ajili ya kuwasaidia na vilevile janga lolote linapotokea humu nchini Wapakistan huchukua hatua zinazostahiki kwa ajili ya kutoa msaada wao kwa wenzao wa Iran kama ilivyoshuhudiwa wazi katika janga la mafuriko la hivi karibuni nchini hapa. Kwa kutilia maanani ukweli huo, safari ya Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan humu nchini inapaswa kutathminiwa kuwa ni hatua nzuri kwa ajili ya kuimarisha uhusiano na kufunguliwa ukurasa mpya wa ushirikiano wa nchi mbili.

Tags