Kiongozi Muadhamu: Iran haitaingia vitani wala kufanya mazungumzo na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i53495-kiongozi_muadhamu_iran_haitaingia_vitani_wala_kufanya_mazungumzo_na_marekani
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amefutilia mbali uwezekano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuingia vitani na Marekani licha ya kushtadi taharuki baina ya pande mbili na kusisitiza kuwa, Washington inafahamu vyema kuwa, kuingia katika vita na Tehran hakutakuwa na maslahi yoyote kwake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 14, 2019 23:28 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Iran haitaingia vitani wala kufanya mazungumzo na Marekani

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amefutilia mbali uwezekano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuingia vitani na Marekani licha ya kushtadi taharuki baina ya pande mbili na kusisitiza kuwa, Washington inafahamu vyema kuwa, kuingia katika vita na Tehran hakutakuwa na maslahi yoyote kwake.

Ayatullah Ali Khamenei aliyasema hayo jana hapa mjini Tehran, wakati alipokutana na wakuu wa mihimili mitatu ya serikali, wabunge pamoja na shakhsia wengine wa ngazi za juu wa kisiasa, kijamii na kiutamaduni.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi hapa nchini amesisitiza kuwa, "Makabiliano kati ya Iran na Marekani hayatakuwa ya kijeshi. Hakuna vita vyovyote vitakavyofanyika."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza bayana kuwa: Chaguo la msingi kwa taifa la Iran mkabala wa Marekani ni muqawama na kusimama kidete, na katika mapambano hayo, hatimaye Marekani italazimika kusalimu amri. 

Ayatullah Khamenei amefafanua kuwa, "Kutokana na vitisho vya Washington, chuki ya Wairani dhidi ya Marekani imeongezeka zaidi ya mara kumi." 

Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote ya Iran amesisitiza kuwa, vikosi vote vya jeshi la Iran viko tayari na viko macho kuzima chokochoko za maadui wakati huu kuliko wakati wowote ule.

Kiongozi Muadhamu na maafisa wa ngazi za juu serikalini

Katika sehemu nyingine katika hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amefutilia mbali pia uwezekano wa kufanyika mazungumzo kati Tehran na Washington kutokana na kile alichokitaja kama mienendo na sera za uhasama na uadui za Marekani kwa taifa hili.

Amesema, "Hakuna afisa yeyote wa Iran mwenye hekima atakubali kufanya mazungumzo kuhusu uwezo mkubwa wa taifa hili; kufanya mazungumzo na serikali ya sasa ya Marekani ni 'sumu hatari yenye kuangamiza'."

Sambamba na kuashiria namna sera za Marekani kwa Ulaya na Asia zimegonga mwamba, Ayatullah Khamenei amebainisha kuwa jamii ya Wamarekani inakabiliwa na changamoto za kiuchumi na kijamii, kutokana na uongozi mbaya na malumbano ya kila siku miongoni mwa maafisa wa serikali ya Washington.