Jeshi la Iran lazindua mfumo wa rada wa Falaq wa ulinzi wa anga
(last modified Sat, 10 Aug 2019 15:29:14 GMT )
Aug 10, 2019 15:29 UTC
  • Jeshi la Iran lazindua mfumo wa rada wa Falaq wa ulinzi wa anga

Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo limezindua mfumo wa rada wa ulinzi wa anga uliopewa jina la Falaq katika hafla iliyohudhuriwa na Kamanda wa Kikosi cha Ulinzi wa Anga cha Jeshi.

Akihutubia katika hafla hiyo, Kamanda wa Kikosi cha Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Brigedia Jenerali Alireza Sabahi-Fard amesema, mfumo huo wa rada unaofika masafa ya kilomita 400 una uwezo wa kugundua na kunasa aina mbali mbali za makombora ya cruise na balestiki pamoja na ndege zinazofanya safari zake kwa kujificha na zisizo na rubani za droni.

Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Sabahi Fard, rada ya ulinzi wa anga ya Falaq ni mfumo wa kisasa unaotokana na mfumo wa kigeni uitwao Gamma, ambao uliingizwa nchini miaka kadhaa iliyopita. Hata hivyo kufuatia vikwazo ilivyowekewa Iran, kutokuwa na vipuri na kushindwa wataalamu wa kigeni kuukarabati mfumo huo, kumewafanya vijana wataalamu wa ndani wa kikosi cha ulinzi wa anga cha jeshi waustawishe mfumo huo na kuongeza kiwango chake cha utendaji, na hatimaye kuuzindua kwa jina la mfumo wa rada wa Falaq.

Aina kadhaa za makombora yaliyoundwa na wataalamu wa Iran

Licha ya kukabiliwa na vikwazo pamoja na mashinikizo ya madola ya Magharibi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepata mafanikio makubwa mno katika sekta ya ulinzi kwa kuweza kujitegemea na kujitosheleza katika uundaji silaha na zana za kijeshi.

Itakumbukwa kuwa tarehe 31 Agosti 2016, wakati Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei alipohutubia hadhara iliyojumuisha Waziri, watafiti na wataalamu wa Wizara ya Ulinzi ya Iran alisisitiza kwa kusema: Katika ulimwengu unaotawaliwa na madola yanayotumia mabavu, ya kibeberu na yenye hisia duni za akhlaqi, dhamiri na utu ambayo hayajali chochote kuvamia nchi zingine na kuua watu wasio na hatia, kustawisha sekta ya ulinzi na ya mashambulizi ni jambo la mantiki kabisa, kwa sababu usalama hautopatikana bila madola hayo kuhisi kuwa Iran ni dola lenye nguvu na uwezo.../

 

Tags