Mafanikio ya sekta ya ulinzi ya Iran; Nguvu kuu na isiyo na shaka katika eneo
(last modified Wed, 21 Aug 2019 12:42:07 GMT )
Aug 21, 2019 12:42 UTC
  • Mafanikio ya sekta ya ulinzi ya Iran; Nguvu kuu na isiyo na shaka katika eneo

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (SEPAH) limetoa taarifa kuadhimisha Siku ya Sekta ya Ulinzi nchini Iran na kuyataja mafanikio katika sekta hiyo ya ulinzi hapa nchini kuwa ni nguvu kuu na isiyo na shaka katika eneo la Asia Magharibi.

Kesho Alhamisi tarehe 22 Agosti ni Siku ya Sekta ya Ulinzi nchini Iran. Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) limeeleza leo katika taarifa yake kwamba, mafanikio na uwezo wa sekta ya ulinzi ya Iran katika nyanja za ardhini, baharini na anga za mbali yaliyopatikana kulingana na viwango vipya vya kimataifa na ambayo ni jibu muafaka kwa vitisho vinavyoikabili nchi hii, yameifanya Iran kuwa dola lenye nguvu zaidi na lisilo na mshindani katika eneo la Asia Magharibi na linaloweza kuchuana na madola ya nje ya eneo hili. Taarifa ya Sepah imeongeza kuwa, kujielekeza na kujikita madola ya kibeberu na kiistikbari duniani katika kubana na kudhibiti nguvu na uwezo wa ulinzi wa Iran ni dhihirisho la wazi la mafanikio na taathira ya kistratejia ya sekta hiyo katika kufelisha njama na senario za harakati ya adui dhidi ya Iran.  

Kuhusiana na suala hilo, nalo Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limesisitiza kupitia taarifa liliyotoa kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Sekta ya Ulinzi nchini Iran kwamba: Vikosi vya ulinzi vya Iran ambavyo vinakabiliwa na vikwazo vya kidhulma na endelevu vya maadui wa mfumo, kwa kutegemea rasilimaliwatu na uwezo wake vyenyewe si tu vimeweza katika kipindi cha miaka 40 kuunda zana zinazohitajika za kujilinda mkabala na vitisho na kuzuia hujuma, bali pia vimefanikiwa kufikia nukta inayohitajika na yenye taathira katika mlingano wa kijeshi na kisiasa katika eneo. 

Jeshi la Sepah katika maneva ya baharini

Wizara ya Ulinzi ya Iran pia imetoa taarifa kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Sekta ya Ulinzi nchini Iran na kueleza kuwa: Kigezo cha nguvu na uwezo wa kiulinzi wa ndani katika medani ya muqawama wa Kiislamu  ni moja ya sababu za kushindwa vita vya niaba, ugaidi na miungano ya kishetani katika Mashariki ya Kati. 

 

 

Tags