Iran: Miungano ya Marekani inasababisha machafuko kote ulimwenguni
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, miungano mbalimbali inayoundwa na Marekani inasababisha machafuko katika kona zote za dunia na kuhatarisha usalama na amani ya kila eneo lenye miungano hiyo.
Sayyid Abbas Mousavi amesema hayo leo ikiwa ni kuonesha hisia zake kuhusu madai ya Marekani ya siku ya Alkhamisi iliyodai kuwa muungano wake wa eti kulinda usalama wa Ghuba ya Uajemi, umeanza kufanya kazi.
Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amegusia jinsi Marekani inavyotumia majina ya nchi nyingine kuhalalisha vitendo vyake vya kiistikbari na kuongeza kuwa, madai hayo ya hivi karibuni ya Marekani yametolewa kwa malengo na tamaa zake zile zile za kila siku za kibeberu na inatumia majina ya nchi nyingine kujaribu kuhalalisha uistikbari wake huo.
Ameongeza kuwa, nchi za eneo hili zinapaswa kutegemea uwezo wao wa ndani, kuishi kwa amani na majirani zao na kushirikiana kieneo kwa ajili ya kuleta usalama wa kudumu, sio kutegemea madola ya kibeberu ambayo hayana nia njema hata chembe na mataifa ya eneo hili.
Aidha amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo ndiyo nchi yenye mpaka mrefu zaidi katika fukwe za Ghuba ya Uajemi, inatumia uwezo wake wote kulinda usalama na manufaa ya kiuchumi yake ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na usalama wa safari za baharini katika eneo hili muhimu sana.