Kiongozi Muadhamu akosoa safari ya kinyemela ya Trump nchini Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i57581-kiongozi_muadhamu_akosoa_safari_ya_kinyemela_ya_trump_nchini_afghanistan
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekosoa vikali safari za kushtukiza na za kificho zinazofanywa na watawala wa Marekani katika nchi za eneo hili la Asia Magharibi kinyume cha sheria.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 30, 2019 04:30 UTC
  • Kiongozi Muadhamu akosoa safari ya kinyemela ya Trump nchini Afghanistan

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekosoa vikali safari za kushtukiza na za kificho zinazofanywa na watawala wa Marekani katika nchi za eneo hili la Asia Magharibi kinyume cha sheria.

Tovuti rasmi ya Ayatullah Ali Khamenei imetuma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter unaosema kuwa, safari hizo za kinyemela katika nchi za eneo hili zinazofanywa na viongozi wa Marekani bila idhini ya serikali husika ni dharau na ukiukaji wa haki na uhuru wa kujitawala nchi za eneo.

Ujumbe huo wa jana Ijumaa wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni radimali kwa safari ya siri iliyofanywa na Rais Donald Trump wa Marekani nchini Afghanistan siku ya Alkhamisi.

Akiwa nchini humo rais huyo wa Marekani alitembelea kambi ya jeshi la Marekani ya Bagram, ambayo ni kambi kubwa zaidi ya jeshi la Marekani nchini Afghanistan, ambapo amekutana na wanajeshi wa taifa hilo la kibeberu. Aidha katika safari hiyo ya ghafla nchini Afghanistan, Rais Donald Trump wa Marekani amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Ashraf Ghani wa nchi hiyo.

Mike Pence alipokutana na wanajeshi wa Marekani walioko nchini Iraq

Kiongozi Muadhamu amebainisha katika ujumbe uliotumwa kwenye tovuti yake rasmi kuwa, "Wamarekani wanakuja katika eneo na kuingia katika nchi kama Iraq bila idhini, huku wakikosa kutembelea mji mkuu wala kukutana na viongozi wa serikali, wanatembelea tu kambi zao kwenye nchi hizo. Huu ni ukiukaji wa uhuru wa kujitawala taifa."

Siku chache zilizopita, Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence aliitembelea Iraq katika safari ya kushtukiza, ambapo aliondoka bila kuutembelea mji mkuu wa nchi hiyo Baghdad, wala kuonana na viongozi rasmi wa serikali.