Iran yaonya; Israel itajuta kuanzisha mashambulizi dhidi ya Syria
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i58079-iran_yaonya_israel_itajuta_kuanzisha_mashambulizi_dhidi_ya_syria
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa ameutahadharisha utawala wa Kizayuni wa Israel, kwa kuanzisha mashambulizi ya anga dhidi ya Syria akisisitiza kuwa, hujuma hizo hazitapita hivi hivi bila kupata jibu kali.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 24, 2019 08:25 UTC
  • Iran yaonya; Israel itajuta kuanzisha mashambulizi dhidi ya Syria

Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa ameutahadharisha utawala wa Kizayuni wa Israel, kwa kuanzisha mashambulizi ya anga dhidi ya Syria akisisitiza kuwa, hujuma hizo hazitapita hivi hivi bila kupata jibu kali.

Ali Akbar Velayati, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu amesema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya Russia Today ya Kiarabu na kubainisha kuwa, mataifa ya Syria na Lebanon yatatoa jibu kali kwa chokochoko hizo za Tel Aviv.

Katika mahojiano hayo ambayo yanatazamiwa kurushwa hewani Jumanne usiku, Velayati amesisitiza kuwa, "Hujuma za anga za Israel dhidi ya Syria hazitapita bila kupata jibu, Tel Aviv itajuta kwa jinai zake hizo."

Amesema ni jambo lisilo na shaka kuwa, vikosi vya Muqawama vya Syria na Lebanon vitajibu mapigo na kusimama kidete dhidi ya jinai hizo za Marekani na utawala haramu wa Israel.

Utawala haramu wa Israel unakiuka anga ya Lebanon katika hujuma zake dhidi ya Syria

Kadhalika Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa amepuuzilia mbali na kuyataja kama propaganda, matamshi yanayotolewa na maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran na kueleza kuwa, "Tel Aviv haina uwezo wala nguvu zozote za kuitishia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."

Ameongeza kuwa, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon itauteketeza na kuubakisha majivu utawala huo pandikizi iwapo utajaribu kuishambulia Lebanon.