Mazoezi ya kijeshi ya Iran, Russia na China yanaendelea kama ilivyopangwa
Mazoezi makubwa ya majeshi ya pamoja ya majeshi ya majini ya Iran, Russia na China leo yameingia siku ya pili na yanaendelea kama ilivyopangwa.
Akizungumza na waandishi habari, Kamanda wa Eneo la Tatu la Jeshi la Majini la Iran Admeli Mustafa Tajuddini amesema mazoezi hayo yanaendelea kwa mafanikio. Ameongeza kuwa, mapema leo manowari za kivita za China na Russia zimeelekea katika eneo la oparesheni kwa ajili ya mazoezi ya ufyatuaji mizinga. Ameongeza kuwa mazoezi hayo yataendelea usiku pia ambapo majeshi hayo yatafanya mazoezi ya kivita katika mazingira ya giza.
Admeli Tajuddini amesema mbali na manowari zake za kivita Russia pia inashiriki katika mazoezi hayo ikiwa na nyambizi tatu nayo China imeleta moja kati ya manoari zake bora zaidi za kivita.
Mazoezi ya Kijeshi ya Iran, Russia na China yalianza jana Ijumaa 27 Disemba na yataendelea kwa muda wa siku nne katika eneo lenye umuhimu wa kistratijia la kaskazini mwa Bahari ya Hindi na Bahari ya Oman.
Amdeli Hussein Khanzadi, Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia mazoezi hayo na kusema: "Mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya Iran, Russia, na China katika Bahari ya Hindi yanafanyika kwa lengo la kuimarisha usalama na misingi yake katika eneo na katika nchi ambazo zina ukuruba kwa mtazamo wa kisiasa, kijamii, kiulinzi na kiusalama.