Tehran yampa Rais wa Ufaransa somo la jiografia kuhusu "Ghuba ya Uajemi"
(last modified Sun, 19 Jan 2020 07:59:39 GMT )
Jan 19, 2020 07:59 UTC
  • Tehran yampa Rais wa Ufaransa somo la jiografia kuhusu

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amempa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa somo la jiografia na kumkosoa kwa kupotosha historia.

Katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwa lugha za Kifarsi, Kifaransa na Kiingereza, Abbas Mousavi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: Namkumbusha Rais Macron kuwa, ghuba inayopatikana kusini mwa Iran ina jina moja tu, nalo ni 'Ghuba ya Uajemi.'

Haya yanajiri siku mbili baada ya Rais Macron kuandika kwenye Twitter kuwa, nchi yake imetuma Kikosi cha Jaguar katika Peninsula ya Uarabuni na Ghuba ya Uarabuni-Uajemi.

Sayyid Mousavi amesema kitendo cha Macron cha kutumia neno hilo ni upotoshaji wa wazi wenye malengo maalumu. Amesema akimhutubu Macron kuwa: Uwepo wenu wa kijeshi katika Ghuba ya Uajemi ni kosa kama ambavyo umelikosea neno lenyewe (Ghuba ya Uajemi). Hayo mawili ni makosa makubwa yanayoweza kufidika.

Ghuba ya Uajemi

Ghuba ya Uajemi, ambayo ni moja ya njia muhimu na za kistratijia za baharini duniani, daima imekuwa chimbuko la fahari kwa taifa la Iran na neno hilo "Ghuba ya Uajemi" limekuwa likitumia katika kipindi chote cha historia na kwenye ramani za kale kwa maelfu ya miaka.

Hata hivyo maadui wasiolipendea mema taifa la Iran wamekuwa wakijaribu kupotosha historia ya kale kwa kuipa jina jipya Ghuba ya Uajemi.