Zarif: Trump amekiri kuwa Iran inalichukia kundi la ISIS
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i59399-zarif_trump_amekiri_kuwa_iran_inalichukia_kundi_la_isis
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema Rais Donald Trump wa Marekani amekiri kuwa askari wa Marekani wako nchini Syria kwa ajili ya kupora mafuta ya nchi hiyo na kwamba Iran inalichukia kundi la kigaidi la ISIS.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 26, 2020 04:23 UTC
  • Zarif: Trump amekiri kuwa Iran inalichukia kundi la ISIS

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema Rais Donald Trump wa Marekani amekiri kuwa askari wa Marekani wako nchini Syria kwa ajili ya kupora mafuta ya nchi hiyo na kwamba Iran inalichukia kundi la kigaidi la ISIS.

Katika ujumbe wa Twitter Jumanne usiku, Zarif alisema: "Trump amekiri kile ambacho sote tulikuwa tunakijua; kwamba wanajeshi wa Marekani wako nchini Syria kwa ajili ya kupora mafuta."

Zarif aidha amesema Trump amekiri kuwa Iran inalichukia kundi la kigaidi la ISIS na kwamba Syria, Russia na Iran zinaweza kupambana na ISIS.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa: "Pamoja na hayo, si tu kuwa Marekani haijapambana na ISIS bali imetekeleza kitendo cha woga na kumuua kigaidi Luteni Jenerali Soleimani, adui nambari moja wa ISIS. Kitendo hicho kilisherehekewa tu na wapambe wa Trump na ISIS.

Akizunguma Jumanne na waandishi habari katika mji mkuu wa India, New Delhi, Trump alidai kuwa Marekani inapambana na ISIS na makundi mengine ya kigaidi Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) na kuongeza kuwa: " Sawa na Marekani, nchi zingine kama vile Iran, Russia, Iraq na Syria zinaweza kupambana na makundi ya kigaidi. Aidha aliiangazia zaidi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema: "Iran inachukia ISIS hivyo inapaswa kupambana na kundi hilo."

Trump amedai kuwa nchi yake inapambana na ISIS katika hali ambayo binafsi huko nyuma ameshawahi kusema kuwa Marekani ndio iliyounda kundi hilo la kigaidi. Katika upande mwingine, nchi za eneo zinakiri kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa katika kupambana na kundi la kigaidi la ISISI nchini Syria na Iraq.

Ikumbukwe kuwa mnamo Januari pili, Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu  na wenzake, waliuawa katika hujuma ya kigaidi ya ndege za kivita za Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Baghdad, Iraq.

Ugaidi huo wa kiserikali wa Marekani umelaaniwa na aghalabu ya nchi za dunia na mashirika ya kimataifa.