Abbas Mousavi: Serikali ya Uingereza haina haki ya kuipangia mambo Iran
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Uingereza haiko katika nafasi ya kutaka kuipangia mambo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Sayyid Abbas Mousavi amesema hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari kwa njia ya video na kusisitiza kuwa, Dominic Raab, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza hana haki wala nafasi ya kuweza kuiainishia mambo Tehran.
Amesema kuwa, uingiliaji wa nchi fulani katika masuala ya mataifa mengine katika maeneo mbalimbali ya dunia hakuna matokeo mengine ghairi ya kuvurugika amani na uthabiti wa nchi husika.
Hivi karibuni Dominic Raab, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza alipuuza wazi mchango wa nchi yake na Marekani katika kuvuruga amani na uthabiti wa Asia Magharibi na kuituhumu Iran kwamba, eti inaendesha harakati za kuvuruga hali ya mambo katika eneo hili. Aidha alidai kwamba, Uingereza haitairuhusu Iran ifanikiwe kuzalisha silaha za nyuklia.
Akijibu matamshi hayo, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kuwa, Tehran daima imekuwa ikikadhibisha madai hayo ya kukaririwa ambayo kiuhakika hayana msingi wowote.
Mousavi amesema, kwa mujibu wa siasa zake, usalama na itikadi yake ya kidini, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hakuna wakati ambao ilifikiria kuunda silaha za nyuklia na imetangaza na kuweka wazi jambo hili mara chungu nzima.
Kadhalika Abbas Mousavi amekumbusha nafasi haribifu ya Uingereza katika kuipatia silaha Saudi Arabia ambazo zinatumika kuwaua raia wasio na hatia wa Yemen na kueleza kwamba, baadhi ya mataifa yanaingilia masuala ya ndani ya Asia Magharibi katika hali ambayo kijiografia yako umbali wa maelfu ya kilomita kutoka katika meneo hili.