Mtihani wa Corona wa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa; kwa maslahi au dhidi ya Iran
(last modified Sat, 11 Apr 2020 04:21:14 GMT )
Apr 11, 2020 04:21 UTC
  • Mtihani wa Corona wa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa; kwa maslahi au dhidi ya Iran

Akijibu hatua za kibaguzi za Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) wakati huu mgumu wa maambukizi ya corona, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa mfuko huo unapasa kutekeleza majukumu yake.

Rais Rouhani amesema: IMF haipasi kuathiriwa na ushetani wa maadui wa taifa la Iran na inalazimika kutekeleza majukumu yake. 

Rais wa Iran, Hassan Rouhani  

Gavana wa Benki Kuu ya Iran, Abdolnaser Hemmati pia amemwandikia barua Mkuu wa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa akieleza matumaini kwamba, katika kipindi hiki nyeti cha historia cha kupambana na corona, upinzani wa Marekani hautakwamisha kazi za kiufundi za IMF na utendaji wake.

Kutoa misaada na mkopo kwa nchi mbalimbali ndiyo kazi muhumu zaidi ya Mfuko wa Fedha wa Kimataifa na mikopo hiyo kimsingi ni miongoni mwa haki za uanachama katika mfuko huo na hutolewa kwa nchi zenye haja. 

Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) una kazi tatu makshsusi na muhimu: Kwanza ni kufuatilia masuala ya kifedha na kiuchumi ya nchi 189 wanachama, pili kutoa ushauri kwa nchi hizo, na tatu kutoa mikopo ya muda mfupi na kuzisaidia nchi zinazokabiliwa na matatizo ya kufedha. 

Katika kipindi hiki virusi vya corona vimeziathiri nchi nyingi duniani na kuna nchi zinazohitajia vyanzo vipya vya fedha kwa ajili ya kupambana na virusi hivyo angamizi; hapa ndipo kazi ya tatu ya Mfuko wa Fedha wa Kimataifa ya kutoa mikopo kwa nchi wanachama zilizoathiriwa na mlipuko wa virusi vya corona inapopata maana yake halisi.

Katika mkondo huo huo IMF mwezi mmoja uliopita baada ya kusambaa virusi vya corona katika nchi mbalimbali duniani ilitangaza utayarifu wake wa kutoa misaada ya haraka na bila ya masharti yoyote kwa nchi wanachama zilizoathiriwa na janga hilo. Baada ya tangazo hilo la IMF Benki Kuu ya Iran ilitaka kutumia haki yake ya kupewa himaya ya kifedha ya mfuko huo lakini inasikitisha kuwa jina la Iran liliondolewa katika orodha ya mwisho ya shirika hilo kwa ajili ya kupokea mkopo.

Matatibu wakiwahudumia wagonjwa wa Corona mjini Tehran 

Kufuatia pingamizi la Marekani, IMF haikutekeleza moja ya majukumu yake muhimu ya kutoa mikopo kwa nchi wanachama ikiwemo Iran na kuonyesha kuwa, badala ya kufanya kazi kiufundi, shirika hilo linaathiriwa na sera na siasa za Marekani. Hii ni licha ya kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa nchi waasisi wa shirika hilo na inasifika kwa kuwa na utendaji mzuri katika masuala ya fedha; hivyo IMF inalazimika kutekeleza majukumu yake ya kisheria. 

Kuhusiana na suala hilo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Masuala ya Kiuchumi, Mohammad Nahavandian siku chache zilizopita aliiambia televisheni ya CNN ya Marekani kwamba: Hakuna nchi yenye haki ya kura ya veto katika Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) na sera za taasisi hiyo ni kufanya insafu katika kutathmini na kupasisha maombi ya nchi wanachama.

Mfuko wa Fedha wa Kimataifa umekhitari kuliondoa jila la Iran katika orodha yake ya mwanzo ya nchi zinazostahiki mkopo baada ya upinzani wa Marekani wakati huu ambapo njia pekee ya kupambana na mlipuko wa virusi vya corona ni mshikamano na majukumu ya pamoja ya dunia nzima. 

Kukubali mashinikizo ya Marekani ambayo inakwamisha jitihada za kimataifa za kupambana na corona, kivitendo kunalifanya shirika hilo lishindwe kutekeleza majukumu yake ya kiufundi. 

Iran ambayo kama tulivyosema ni miongoni mwa nchi waasisi wa IMF na yenye utendaji safi na wa wazi katika masuala ya kifedha, katika kipindi hiki iko mstari wa mbele katika mapambano ya dunia dhidi ya mlipuko wa virusi vya corona, na hapana shaka kuwa, misaada na ushirikiano wa mfuko huo utaboresha mapambano hayo na kuzidisha kasi na taathira ya vita vya dunia nzima dhidi ya ugonjwa wa COVID-19. 

Tags