Jeshi la Majini la Iran kuunda nyambizi za nyuklia
(last modified Fri, 17 Apr 2020 04:30:03 GMT )
Apr 17, 2020 04:30 UTC
  • Jeshi la Majini la Iran kuunda nyambizi za nyuklia

Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kikosi hicho kinajiandaa kuunda nyambizi zitakazotumia nishati ya nyuklia zenye uwezo wa kutekeleza operesheni za baharini kwa muda mrefu zaidi katika maji ya kimataifa.

Admeri Hossein Khanzadi alisema hayo jana Alkhamisi na kufafanua kuwa, ni katika ajenda kuu ya Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuunda nyambizi zinazotumia nishati ya nyuklia, na kwamba hakuna nguvu au dola lolote linaloweza kuizuia Iran kustafidi na nishati yake ya nyuklia kwa malengo ya kujidhaminia amani na usalama.

Admeri Khanzadi amesisitiza kuwa, msimamo wa Iran juu ya kustafidi na nishati ya nyuklia upo wazi, na kwamba Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mara kwa mara amekuwa akisisitizia malengo ya amani ya miradi ya nyuklia ya taifa hili yenye malengo ya amani. Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia mafanikio ya kikosi hicho katika uundaji anuai za vyombo na zana za majini na kueleza kwamba, lengo la hatua hiyo ni kudhamini usalama na kuhakikisha kunakuwepo ulinzi kamili katika maeneo ya pwani ya Iran.

Nyambizi ya Fateh ya Iran

Mwaka jana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilizindua nyambizi ya kisasa iliyoundwa hapa nchini ambayo ina uwezo wa kusheheni makombora ya cruise. Kabla ya hapo pia, Iran ilizindua nyambizi mbili za Ghadir ambazo zina uwezo wa kurusha makombora kutoka chini ya bahari. Katika miaka ya hivi karibuni, Iran imeweza kuzindua nyambizi kadhaa za kisasa zilizoundwa humu nchini kama vile Qaem, Nahang, Tareq, Fateh na Sina.

Admeri Hossein Khanzadi, Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Tags