Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran akutana na Rais wa Syria
(last modified Mon, 20 Apr 2020 12:04:16 GMT )
Apr 20, 2020 12:04 UTC
  • Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran akutana na Rais wa Syria

Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ambaye leo amefanya safari ya siku moja nchini Syria amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa nchi hiyo Bashar al-Assad ambapo wawili hao wamejadili masuala mbalimbali ya pande mbili, kieneo na kimataifa.

Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa na viongozi hao ni matukio ya hivi karibuni ya kisiasa na vita dhidi ya ugaidi nchini Syria.

Baadhi ya duru zinasema kuwa, moja ya mada kuu katika mazungumzo ya Rais Bashar al-Assad na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ni kuhusiana na duru ijayo ya mazungumzo ya Astana ambayo ni maalumu kwa ajili ya kujadili kadhia ya Syria.

Duru ijayo ya mazungumzo ya Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Russia na Uturuki ambao ndio wadau wakuu mazungumzo hayo inatarajiwa kufanyika Jumatano ijayo.

Ujumbe wa Iran unaoongozwa na Waziri wa Mashauri ya Kigeni Dakta Muhammad Javad Zarif ukiwa katika mazungumzo mjini Damascus na ujumbe wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Syria

Akiwa mjini Damascus, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikutana na kufanya mazungumzo pia na Walid al-Muallim Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Syria.

Maandamano ya kupinga serikali yalianza nchini Syria tarehe 15 Machi 2011 kwa sura ya kufuata mkumbo wa yale yaliyokuwa yakijiri katika nchi zingine za Kiarabu. Hata hivyo tofauti kubwa zaidi kati ya matukio ya Syria na yaliyotokea katika nchi nyingine za Kiarabu ni kwamba, malalamiko ya upinzani wa ndani nchini Syria yaligeuka kuwa vita kati ya mfumo wa utawala wa nchi hiyo na makundi ya kigaidi, kutokana na uingiliaji wa mhimili wa pande nne za Wamagharibi, Waarabu, Waebrania na Waturuki.