Walimwengu wapaza sauti kulaani mauaji ya mwanasayansi wa nyuklia wa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i64909-walimwengu_wapaza_sauti_kulaani_mauaji_ya_mwanasayansi_wa_nyuklia_wa_iran
Mataifa na viongozi mbalimbali wa dunia wameendelea kulaani mauaji ya mwanasayansi wa nyuklia wa Iran na kusisitiza kuchukuliwa hatua waliohusika na jinai hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 29, 2020 04:20 UTC
  • Walimwengu wapaza sauti kulaani mauaji ya mwanasayansi wa nyuklia wa Iran

Mataifa na viongozi mbalimbali wa dunia wameendelea kulaani mauaji ya mwanasayansi wa nyuklia wa Iran na kusisitiza kuchukuliwa hatua waliohusika na jinai hiyo.

Faisal Mekdad, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Syria amelaani mauaji ya mwanasayansi wa nyuklia wa Iran katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na kuitaka jamii ya kimataifa itekeleze majukumu yake ipasavyo kuhusiana na vitendo vya kigaidi kama hivi.

Muhammad Bin Abdul-Rahman Al-Thani, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar naye amelaani mauaji ya kigaidi ya Mohesn Fakhrizadeh mwanasayansi wa nyuklia wa Iran na kubainisha kwamba, katika hali ambayo kunafanyika juhudi za kupunguza mizozo na mivutano katika eneo la Asia Magharibi, kuuawa mwanasayansi huyu wa nyuklia kutazidi kuchochea moto wa machafuko.

Wakati huo huo, Mustafa Sentop, Spika wa Bunge la Uturuki amelaani mauaji ya mwanasayansi huyo na kuitaja hatua hiyo kuwa ni ya kigaidi.

Shahidi Mohsen Fakhrizadeh

 

Aidha Ismail Hania, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Dakta Zarif na kulaani vikali mauaji hayo aliyotaja kuwa ni ya kigaidi.

Kwa upande wake, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon sambamba na kulaani mauaji ya mwanasayansi wa nyuklia wa Iran imesisitiza kuwa, iko pamoja na taifa la Iran kwa ajili ya kukabiliana na vitisho na njama za maadui.

Mohsen Fakhrizadeh, Mkuu wa Shirika la Utafiti na Ubunifu la Wizara ya Ulinzi ya Iran aliuawa shahidi Ijumaa iliyopita katika shambulio la kigaidi lililofanywa katika viunga vya jiji la Tehran.