Oman yatoa mkono wa pole kwa serikali na wananchi wa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i64917-oman_yatoa_mkono_wa_pole_kwa_serikali_na_wananchi_wa_iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman ametoa mkono wa pole kwa serikali na wananchi wa Iran baada ya kuuawa kigaidi, mwanasayansi mkubwa wa nyuklia na masuala ya kijeshi wa Iran, shahidi Mohsen Fakhrizadeh.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Nov 30, 2020 01:05 UTC
  • Oman yatoa mkono wa pole kwa serikali na wananchi wa Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman ametoa mkono wa pole kwa serikali na wananchi wa Iran baada ya kuuawa kigaidi, mwanasayansi mkubwa wa nyuklia na masuala ya kijeshi wa Iran, shahidi Mohsen Fakhrizadeh.

Magaidi wenye silaha, siku ya Ijumaa waliishambulia gari la Dk Mohsen Fakhrizadeh, Mkuu wa Taasisi ya Utafiti na Ubunifu katika Wizara ya Ulinzi ya Iran na kumuua shahidi mwanasayansi huyo wa teknolojia ya nyuklia ambaye alikuwa mstari wa mbele pia katika kupambana na ugonjwa wa COVID-19.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Bw. Badr bin Hamad al Busaidi amezungumza kwa simu na waziri mwenzake wa Iran, Dk Mohammad Javad Zarif na kulaani mauaji hayo ya kigaidi. Katika mazungumzo hayo ya simu, al Busaidi ametoa mkono wa pole kwa serikali na wananchi wa Iran na kusema kuwa Oman inapinga ugaidi wa aina yoyote ile na inaamini kuwa ni kitu kisichokubalika kabisa.

Shahid Mohsen Fakhrizadeh

 

Kabla ya hapo pia, Faisal Mekdad, Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria alikuwa amelaani mauaji ya mwanasayansi wa nyuklia wa Iran katika mazungumzo yake ya simu na Dakta Muhammad Javad Zarif, na kuitaka jamii ya kimataifa itekeleze majukumu yake ipasavyo kuhusiana na vitendo vya kigaidi kama hivyo.

Muhammad Bin Abdul-Rahman Aal Thani, Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar naye amelaani mauaji ya kigaidi ya shahid Mohsen Fakhrizadeh na kubainisha kwamba, kuuawa mwanasayansi huyu wa nyuklia wa Iran kutazidi kuchochea moto wa machafuko hasa wakati huu ambapo kunafanyika juhudi za kupunguza mizozo na mivutano katika eneo la Asia Magharibi. Kwa upande wake, Mustafa Sentop, Spika wa Bunge la Uturuki naye amelaani mauaji ya mwanasayansi huyo na kuitaja hatua hiyo kuwa ni ya kigaidi.