Zarif: Mjumbe wa Iran UN hajazungumza na Marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa hajafanya mazungumzo yoyote na Marekani kama lilivyodai gazeti moja la Ufaransa.
Mohammad Javad Zarif alisema hayo jana Jumatano na kuongeza kuwa, Majid Takht-Ravanchi, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran UN amekuwepo hapa mjini Tehran kwa muda wa wiki tatu, na kwa msingi huo madai ya gazeti la Le Figaro hayana ukweli wowote.
Gazeti hilo la Ufaransa lilidai kuwa Takht-Ravanchi alikutana na kufanya mazungumzo na timu ya Rais mpya wa Marekani, Joe Biden mjini Washington.
Kuhusu uwezekano wa kufanya mazungumzo mapya juu ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA, Dakta Zarif ameeleza bayana kuwa: Tuna makubaliano ya nguvu na ni muhali kuyajadili upya.
Amesema utawala wa Donald Trump umeingia katika jaa la taka za historia, huku akiuasa utawala mpya wa Marekani utekeleze wajibu wake na kuiondolea vikwazo Jamhuri ya Kiislamu.
Kadhalika Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amezikosoa nchi za Ulaya kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ili kuyalinda mapatano ya nyuklia akisisitiza kuwa, "Ulaya inafahamu kuwa, nchi pekee ambayo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita imeheshimu JCPOA kwa maslahi ya wananchi wake na maslahi ya jamii ya kimataifa ni Iran. Ulaya haijafanikiwa kutekeleza hata jukumu dogo la INSTEX."
Tangu mfumo wa INSTEX uzinduliwe mwezi Aprili mwaka jana, nchi za Ulaya zimefeli kuthibitisha kuwa mfumo huo wa mabadilishano ya kifedha na Iran unafanya kazi ili Iran iweze kunufaika kiuchumi na mapatano ya nyuklia ya JCPOA.