IRGC yazionya nchi za eneo zinazofanya urafiki na Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i66618-irgc_yazionya_nchi_za_eneo_zinazofanya_urafiki_na_israel
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran (IRGC) ameonya kuwa, uwepo wa utawala wa Kizayuni katika eneo la Asia Magharibi hautaliletea eneo hili kitu kingine ghairi ya 'moto.'
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 08, 2021 08:47 UTC
  • IRGC yazionya nchi za eneo zinazofanya urafiki na Israel

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran (IRGC) ameonya kuwa, uwepo wa utawala wa Kizayuni katika eneo la Asia Magharibi hautaliletea eneo hili kitu kingine ghairi ya 'moto.'

Meja Jenerali Ali Baqeri amesema hayo leo Jumatatu katika hafla ya Kikosi cha Majini cha IRGC ya kupokea boti 340 za kivita zenye uwezo wa kuvurumisha makombora katika mji bandari wa Bandar Abbas, ambapo amezionya nchi za eneo zinazofanya urafiki na kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo wa Kizayuni.

Ameyahutubu madola ya eneo hili yanayojikomba kwa Israel akiyaambia kuwa: Wazayuni ni sawa na mti uliolaaniwa, ambao hauzai chochote isipokuwa moto.

Meja Jenerali Baqeri ameeleza bayana kuwa, kitendo cha nchi vibaraka katika eneo cha kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni kinathibitisha wazi chuki zao dhidi ya Waislamu.

Amesisitiza kuwa, Marekani si dola lenye nguvu kubwa duniani tena, na kwamba hivi sasa haiwezi kueneza sera zake popote inapotaka duniani.

Boti za kisasa za kivita za IRGC ya Iran

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, Wamarekani wanapaswa kutambua kuwa sera zao za mashinikizo dhidi ya taifa hili zimegonga mwamba, na kosa hilo halifai kukaririwa na utawala mpya wa Washington.

Meja Jenerali Salami ameongeza kuwa, katu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiwezi kuuza mamlaka na uhuru wake wa kujitawala kutokana na vikwazo, na kwamba taifa hili limesimama kidete na litakabiliana na matokeo hasi ya mashinikizo hayo ya maadui.