Admeri Sayyari: Adui anaogopa uwezo wa kujihami wa Iran
(last modified Sun, 21 Feb 2021 07:49:01 GMT )
Feb 21, 2021 07:49 UTC
  • Admeri Sayyari: Adui anaogopa uwezo wa kujihami wa Iran

Naibu Mratibu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema adui anatiwa hofu na uwezo mkubwa wa kiulinzi wa taifa hili akifahamu fika kuwa, iwapo atajaribu kufanya kosa lolote, basi atakabiliwa kwa jibu kali.

Admeri Habibullah Sayyari amesema hayo leo Jumapili na kuongeza kuwa, kulinda mipaka na mamlaka ya kujitawala nchi hii ni wajibu wa kila Muirani, kama ambavyo taifa zima lilijitokeza kupambana katika vita vya miaka minane vya kulazimishwa dhidi ya Iraq (1980-1988).

Amesema wananchi Waislamu wa Iran walijitokeza kwa makundi katika vita hivyo vya kujihami kutakatifu, ili kuhakikisha kuwa Mapinduzi ya Kiislamu yanalindwa. 

Mratibu wa jeshi la Iran ameashiria pia utayari wa vikosi vya ulinzi vya Iran wa kukabiliana na kitisho cha aina yoyote ile na akasisitiza kwa kusema: Iran haina nia yoyote ya kuanzisha uchokozi kwenye mipaka na dhidi ya maslahi ya nchi zingine, lakini kama itatokea wakati ikahitajika kuonyesha nguvu na uwezo wake wa kijeshi ili kutokomeza vitisho dhidi yake, bila shaka yoyote itafanya hivyo.

Majaribio ya makombora ya balestiki ya Iran

Admeri Habibullah Sayyari amebainisha kuwa, kwa muda wote wa zaidi ya miaka 40 tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, zana za ulinzi za vikosi vya ulinzi vya Iran zimekuwa zikiundwa hapa nchini na ubora wake hauwezi kulinganishwa na wa kabla ya mapinduzi.

Naibu Mratibu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza bayana kuwa, maadui wanafanya juu chini kuhakikisha wanarejea hapa nchini, na katika miaka ya hivi karibuni, wamefanya operesheni nyingi za kijeshi mashariki na magharibi mwa nchi ili kuwatisha wananchi wa Iran. Amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu haibabaishwi na vitisho hivyo na itatoa jibu kali kwa chokochoko zozote za maadui dhidi yake.

 

Tags