Meja Jenerali Salami: Iran iko tayari kukabiliana na vitisho vya adui
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema vikosi vya ulinzi vya Iran vimejiandaa na vipo tayari kukabiliana na vitisho na chokochoko za maadui.
Meja Jenerali Hussein Salami amesema hayo kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuuawa shahidi, Meja Jenerali Ali Sayyad Shirazi, aliyekuwa Kaimu Kamanda Mkuu wa Majeshi yote na mmoja wa makamanda shupavu wa jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, baada ya kufyatuliwa risasi na vibaraka wa kundi la kigaidi la Munafiqiin mjini Tehran, katika siku kama ya leo miaka 22 iliyopita.
Meja Jenerali Salami ameeleza bayana katika taarifa aliyoitoa kwa mnasaba wa kumbukizi hiyo kuwa, kuuawa shahidi ni nembo ya izza na utukufu kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) ameongeza kuwa, taifa hili litaendelea kusimama kidete mkabala wa uhasama na mashinikizo ya maadui.
Meja Jenerali Shirazi alikuwa mwanaharakati wa mapinduzi, na alitupwa gerezani mara kadhaa wakati wa utawala wa Shah, na hatimaye aliachiliwa huru baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Aliuawa shahidi tarehe 21 Farvardin 1378 Hijria Shamsia sawa na April 10 mwaka 1999 na vibaraka wa MKO hapa mjini Tehran. Meja Jenerali Sayyad Shirazi aliwahi kuwa Kamanda wa Jeshi la Nchi kavu wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran.