Larijani: Kuunga mkono magaidi ni kwa maslahi ya Wazayuni
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i6919-larijani_kuunga_mkono_magaidi_ni_kwa_maslahi_ya_wazayuni
Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran amezikosoa baadhi ya nchi katika eneo hili la Mashariki ya Kati kwa kuyaunga mkono makundi ya kigaidi na kusisitiza kuwa kuungwa mkono ugaidi ni kwa maslahi ya Wazayuni.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 12, 2016 07:20 UTC
  • Larijani: Kuunga mkono magaidi ni kwa maslahi ya Wazayuni

Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran amezikosoa baadhi ya nchi katika eneo hili la Mashariki ya Kati kwa kuyaunga mkono makundi ya kigaidi na kusisitiza kuwa kuungwa mkono ugaidi ni kwa maslahi ya Wazayuni.

Akiongea katika duru ya 33 ya Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu iliyoanza hapa mjini Tehran jana Jumatano, Ali Larijani amesema baadhi ya nchi zinazojiita kuwa za Kiislamu katika eneo ni maadui wa Mwenyezi Mungu kwa kuwa zinaunga mkono kuuawa na kudhulumiwa kwa Waislamu katika nchi kama Yemen na Syria.

Spika wa Bunge la Iran ameongeza kuwa: "Kwa kuyaunga mkono makundi ya kigaidi, serikali za nchi hizo zimeunga mkono kumwagwa damu za Waislamu na kwamba, anayefaidika na ukatili huo ni Mzayuni."

Ali Larijani ameeleza kusikitishwa kwake na namna nchi hizo zinazodai kuwa za Kiislamu zinavyochapisha Qur'ani Tukufu ilhali zimeshindwa kabisa kufuata mafundisho ya Kitabu hicho Kitakatifu.

Mashindano ya 33 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran yalianza jana Jumatano katika Ukumbi Mkubwa wa Swala wa Imam Khomeini MA na yanatazamiwa kuendelea hadi Mei 17.

Sheikh Ali Mohammadi, Mwakilishi wa Faqihi Mtawala na Mkuu wa Shirika la Awqaf la Iran amesema kuna washiriki 130 kutoka nchi 75 duniani ambao wanashiriki katika mashindano hayo ya kila mwaka.