Kiongozi Muadhamu asikitishwa na kifo cha Shahidi Jenerali Hijazi
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mkono wa pole na kueleza juu ya kusikitishwa kwake na kifo cha Brigedia Jenerali Mohammad Hosseinzadeh Hijazi, Naibu Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ambaye ameaga dunia usiku wa kuamkia leo akiwa na umri wa miaka 65, kutokana na mshtuko wa moyo.
Katika salamu hizo za pole, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema amesikitishwa mno na habari ya kuaga dunia Jenerali Hijazi, ambapo amemuombea amani na baraka za Allah.
Kiongozi Muadhamu amemuomba Mwenyezi Mungu ampe faraja mjane, watoto, familia na wafanyakazi wenza za Shahidi Hijazi, katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Amesema miongoni mwa sifa na tabia alizojipamba nazo Jenerali Hijazi ni moyo wa kujitolea na kupambana, fikra pevu, moyo uliojaa imani ya kweli na ilhamu. Ayatullah Ali Khamenei amesema Brigedia Jenerali Hijazi alisabilia maisha yake katika kuuhudumia Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu.
Mwishoni mwa ujumbe huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amemuomba Allah amrahamu na kumsamehe madhambi yake Jenerali Hijazi.
Wakati huo huo, Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amemtumia ujumbe wa rambirambi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, kufuatia kifo cha Shahidi Hijazi.
Katika ujumbe huo, Sayyid Nasrullah amesema amesitikishwa mno na kifo cha ghafla cha shujaa huyo wa mapambano.