Majina ya wagombea urais nchini Iran, yatajwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i70540-majina_ya_wagombea_urais_nchini_iran_yatajwa
Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetaja majina ya wagombea wa urais katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao wa Juni humu nchini.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 25, 2021 11:06 UTC
  • Majina ya wagombea urais nchini Iran, yatajwa

Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetaja majina ya wagombea wa urais katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao wa Juni humu nchini.

Katika taarifa yake ya leo Jumanne, tume ya uchaguzi ya Iran imetangaza majina ya wagombea katika uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliotimiza masharti ya kugombea kwa mujibu wa sheria za uchaguzi za Jamhuri ya Kiislamu.

Taarifa hiyo imesema, katika utekelezaji wa kifungu cha 60 cha sheria ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu, majina ya wagombea wa uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliotimiza masharti na kupasishwa na Baraza la Kulinda Katiba ni kama ifuatavyo:

Saeed Jalili, Mohsen Rezaee Mirgha'ed, Sayyid Ebrahim Raisol-Sadati (Ebrahim Raisi), Alireza Zakani, Sayyid Amir-Hossein Ghazizadeh Hashemi, Mohsen Mehralizadeh na Abdolnaser Hemmati.

Uchaguzi ni sehemu muhimu mno katika mfumo wa demokrasia ya kidini nchini Iran

 

Kwa mujibu wa kifungu cha 66 cha sheria, kampeni za uchaguzi za wagombea wa urais zinaanza rasmi siku na tarehe ya kutangazwa majina ya wagombea na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran. Kampeni hizo zinaendelea hadi masaa 24 kabla ya kuanza zoezi la kupiga kura.

Wagombea wote nchini Iran wanapewa haki sawa kwa kuhesabiwa mpaka sekunde za kufanya kampeni katika vyombo vya habari vya taifa kama vile redio na televisheni, bila ya kupunguziwa au kuongezewa hata sekunde moja.

Uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na uchaguzi wa 6 wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji unatarajiwa kufanyika Ijumaa ya tarehe  18 mwezi ujao wa Juni, 2021.