Jun 04, 2021 09:35 UTC
  • Taathira za fikra za Imam Khomeini MA katika eneo la Asia Magharibi

Ijumaa ya leo ya tarehe 4 Juni imesadifiana na mwaka wa 32 wa kufariki dunia mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran. Moja ya maudhui muhimu zinazozungumziwa leo hii ni taathira za fikra na sira ya Imam Khomeini MA katika eneo zima la Asia Magharibi.

Imam Khomeini MA alidhihiri akiwa kiongozi wa Iran katika wakati ambao, kwanza Iran ilikuwa mtekelezaji wa siasa za madola ya Magharibi hasa Marekani katika eneo hili, na ilikuwa polisi wa nchi hizo Asia Magharibi. Pili udhaifu wa nchi za Kiarabu mbele ya utawala wa Kizayuni ulikuwa umejitokeza wazi kutokana na mkataba wa Camp David. Tatu rai za wananchi hazikuwa na maana wala thamani yoyote katika maamuzi ya kisiasa na kiutawala ya nchi za eneo la Asia Magharibi. Sasa tunapozungumzia taathira za fikra za Imam Khomeini MA katika masuala ya eneo la Asia Magharibi hatuwezi kabisa kukwepa kuzingatia mambo hayo matatu muhimu.

Kwa kupata ushindi Mapinguzi ya Kiislamu nchini Iran yaliyongozwa na Imam Khomeini MA, si tu Iran ilijipapatua kutoka katika hali ya kuwa polisi wa madola ya Magharibi kwenye eneo hili, lakini pia Iran ambayo ni nchi muhimu sana, ilibadilika na kuwa mpinzani mkubwa wa siasa za kibeberu za madola hayo hasa Marekani. Baada ya kupita takriban miaka 43 tangu kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran, hivi sasa moyo na hisia za kuipinga Marekani katika eneo la Asia Magharibi zimeongezeka sana huku mataifa ya eneo hili yakionesha waziwazi hamu yao ya kutimuliwa wanajeshi wa Marekani katika nchi zao. Hiyo ndiyo hamu ya idadi kubwa ya Waislamu sasa hivi na bila ya shaka yoyote, hayo ni katika matunda ya kuenea fikra za Imam Khomeini katika eneo hili.

Baadhi ya harakati za muqawama wa Kiislamu Asia Magharibi

 

Taathira nyingine muhimu ya fikra za Imam Khomeini katika eneo la Asia Magharibi ni kuundwa kambi ya muqawama ya kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel. Mapinduzi ya Kiislamu yalipata ushindi nchini Iran wakati ambapo Misri ilikuwa imetia saini mkataba wa Camp David na kufungua mlango wa kujidhalilisha nchi za Kiarabu kwa utawala wa Kizayuni na mabwana zake. Mkataba huo ulitia nguvu ngano iliyokuwa imepandikizwa ya kwamba jeshi la Israel halishindiki na ulikuwa na maana ya kulipiga teke na kulitupa suala zima la Palestina.

Hata hivyo Imam Khomeini alipofanikisha Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran alizidi kuweka wazi msimamo wake usiotetereka wa kuwatetea Wapalestina. Alitangaza wazi kuwa Israel ni donda ndugu la kensa na alifanya ubunifu wa kipekee kabisa wa kuitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds ambayo imetoa pigo kubwa kwa kambi ya nchi zinazojidhalilisha kwa Wazayuni kupitia mapatano yao yasiyo na maana. Kwa ubunifu wake huo, Imam Khomeini aliirejesha kadhia ya Palestina katika masuala muhimu mno ya Ulimwengu wa Kiislamu. Wakati huo huo alikuja na fikra ya kuanzisha kambi ya muqawama kupitia kuziunga mkono harakati mbalimbali zinazopigania ukombozi na kupambana na utawala wa Kizayuni katika eneo hili. Kuundika makundi ya muqawama huko Palestina na Lebanon kulikuwa na maana ya kuanza mchakato wa kupambana kiistratijia na kwa malengo maalumu na Israel. Leo hii, wananchi wa Palestina hawakabiliani tena kwa mawe na utawala wa Kizayuni, bali wanapambana nao kwa makombora. Abdullah Ganji, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: Kuifanya Siku ya Quds kuwa ya kimataifa kulifanyika kwa lengo la kuhakikisha kuwa Waislamu hawakisahau wala kukipuuza Kibla chao cha Kwanza yaani Msikiti wa al Aqsa. Pia kulifanya suala la Palestina lisisahauliwe na jambo hilo limeweza kuitoa kadhia hiyo kutoka katika mgogoro wa Palestina na Mayahudi au Waarabu na Wazayuni na sasa hivi suala la Palestina limekuwa ni mapambano baina ya Ulimwengu wa Kiislamu na Magharibi.

Sasa wanamapambano wa Palestina hawapambani tena kwa mawe, wanamapambana na Israel kwa makombora

 

Taathira nyingine muhimu ya fikra ya Imam Khomeini ni kuasisi kwake mfumo wa demokrasia ya kidini katika eneo la Asia Magharibi ili kuwatangazia walimwengu kuwa kura na maamuzi ya wananchi yana umuhimu mkubwa katika maamuzi ya kila nchi. Fikra hiyo imeziamsha fikra za wananchi wa Ulimwengu wa Kiislamu kiasi kwamba sasa hivi wananchi wa nchi hizo mara kwa mara wamekuwa wakitangaza wazi hamu yao ya kuwa na nafasi katika maamuzi ya nchi zao. Mapinduzi ya wananchi yaliyotokea katika nchi za Kiarabu kuanzia mwaka 2011, bila ya shaka yoyote yameathiriwa na fikra hizo za Imam Khomeini MA. 

Kiujumla ni kwamba, fikra za Imam Khomeini MA zimepelekea kuundika mfumo mpya Asia Magharibi uliosimama juu ya msingi wa kupinga uingiliaji wa madola ya kigeni, wajibu wa kila nchi kuwa na ulinzi unaotegemea nguvu zake za ndani, kuundika makundi ya muqawama yenye nguvu na aidha kulazimika watawala wa nchi za eneo hili kutilia maanani na kujali mitazamo ya wananchi wao katika mifumo yao ya kisiasa. 

Tags