Jul 25, 2021 01:22 UTC
  • Iran yasajili chanjo yake ya Corona COVIran Barekat katika WHO

Mchakato wa kusajili chanjo ya kuzuia ugonjwa wa COVID-19 iliyoundwa hapa nchini Iran ya COVIran Barekat katika Shirika la Afya Duniani (WHO) umeanza.

Dakta Asghar Abdoli, Profesa Msaidizi na mjumbe wa Bodi ya Taasisi ya Chanjo ya Pasteur ya Iran (IPI) alitangaza hayo jana Jumamosi na kueleza kuwa, mbali na kuwasilisha nyaraka za kisayansi zinazohusu mchakato mzima wa utengenezaji wa chanjo hiyo, lakini watatakiwa pia kujiwasilisha wenyewe mbele ya WHO ili kutetea nyaraka hizo.

Dakta Abdoli amebainisha kuwa, makala ya kwanza ya majaribio ya kabla ya kliniki (wanyama) ya chanjo ya COVIran Barekat itachapishwa karibuni hivi. 

Afisa huyo mwandamizi wa Taasisi ya Chanjo ya Pasteur ya Iran ameongeza kuwa, dozi milioni mbili za chanjo ya COVIran Barekat zitakuwa tayari kwa ajili ya matumizi wiki ijayo.

Chanjo ya Corona ya COVIran Barekat ni matunda ya wahakiki na wanasayansi vijana wa Iran ambayo hivi karibuni iliidhinishwa kuanza kutumiwa kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa wa COVID-19.

Iran kuanza kuzalisha kwa wingi chanjo ya Corona ya COVIran Barekat

Kuzinduliwa chanjo hiyo kunaiweka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika orodha ya nchi sita tu duniani zinazotengeneza chanjo za Corona. Tayari nchi 12 zikiwemo za Ulaya, Asia na Amerika ya Latini zimewasilisha maombi ya kutaka kuagiza chanjo ya COVIran Barekat.

Iran iko mbioni kuunda chanjo kadhaa za COVID-19, ambapo mbali na  chanjo ya hiyo COVIran Barekat, chanjo zingine ambazo zimepiga hatua nzuri katika majaribio ni pamoja na Razi Cov Pars,  Fakhra na chanjo ya pamoja ya Taasisi ya Chanjo ya Finlay ya Cuba na Taasisi ya Chanjo ya Pasteur ya Iran.

Tags