Iran: Inawezekana kufikia makubaliano mazuri katika mazungumzo ya Vienna
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza matumaini yake ya kufikiwa mapatano ya kuridhisha katika mazungumzo ya nyuklia ya Iran na kundi la 4+1 linaloundwa na mataifa ya Russia, China, Uingereza, Ufaransa pamoja Ujerumani yanayoendelea huko Vienna, Austria.
Hossein Amir-Abdollahian alisema hayo jana Jumanne pambizoni mwa marasimu ya kumuenzi aliyekuwa balozi wa Iran nchini Yemen, Hasan Irloo na kuongeza kuwa, "mazungumzo yako katika njia sahihi, kufikiwa makubaliano ni kitu kinachowezekana iwapo upande wa pili wa mazungumzo utakuwa na nia na irada njema ya kisiasa."
Amir-Abdollahian amebainisha kuwa, timu ya Iran kwenye mazungumzo hayo kwa sasa inajishughulisha zaidi na suala la kufikiwa matini ya pamoja ya makubaliano ambayo yanaziridhisha pande zote husika.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza bayana kuwa, makubaliano juu ya nukta zenye utata kwenye matini ya mapatno hayo yatafikiwa katika kipindi kifupi kiijacho, iwapo upande wa pili utafanya mazungumzo kwa dhati na nia njema.
Duru ya nane ya mazungumzo ya Vienna yanayoangazia suala la kuondolewa vikwazo vya kidhalimu na haramu dhidi ya Iran ilianza juzi Jumatatu kwa kikao cha Kamisheni ya Pamoja iliyoongozwa na Ali Bagheri, mkuu timu ya mazungumzo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Enrique Mora, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Huduma ya Kigeni Umoja wa Ulaya.