Jan 02, 2022 08:08 UTC
  • Kamanda wa IRGC adungwa chanjo ya COVID-19 ya Noora ya Iran

Chanjo nyingine ya COVID-19 iliyotegenezwa Iran ijulikanayo kama Noora imeingia awamu ya tatu ya majaribio kwa mwanaadamu kwa kudungwa Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).

Awamu hii ya tatu ya majaribio ya chanjo hiyo ya Noora imeanza Jumapili katika hafla iliyofanyika mjini Tehran na kuhudhuriwa na Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Meja Jenerali Hossein Salami na Waziri wa Afya Daktari Bahran Einollahi. Hafla hiyo imefanyika kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mwaka wa pili wa kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani. Watu 10,000 waliojitolea watadungwa chanjo hiyo.

Meja Jenerali Salami amedungwa chanjo hiyo akiwa miongoni mwa waliojitolea katika awamu hii ya ya tatu ya majaribio ya chanjo ya Noora.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Baqiyatullah Daktari Hassan Abulqasemi amesema chanjo milioni tano zitazalishwa na chuo hicho kwa kushirikiana na IRGC na kukabidhiwa wizara ya afya punde baada ya awamu ya tatu ya majaribio kwa mwanadamu kukamilika.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Afya Daktari Einollahi amesema wananchi wa Iran wameonyesha uwezo wao wa kukabiliana na janga la COVID-19 katika kipindi cha miezi minne iliyopita. Amesema katika kipindi hicho Iran imeweza kudunga dozi milioni 120 za COVID-19.

Iran iko katika mstari wa mbele kutengeneza chanjo za COVID-19 ambapo mbali na chanjo ya Noora  pia sasa imezalisha chanjo ya COV Iran Barakat ambayo kwa miezi kadhaa imekuwa ikitumika kwa mafanikio katika zoezi la chanjo nchini. Chanjo  nyingine ambayo imetengenezwa Iran na sasa inatumika katika zoezi la chanjo ni ile ya PastoCoVac ambayo nayo pia hivi karibuni imeanza kutumika katika zoezi la chanjo.

Chanjo hizo tatu za Iran sasa zinasubiri kibali cha Shirika la Afya Duniani ili kuanza kuuzwa katika soko la kimataifa. Pamoja na hayo nchi kadhaa duniani zimeshaagiza chanjo hizo za Iran. Chanjo nyingine ya Iran ambayo inatazamiwa kuzinduliwa hivi karibuni ni ile ya Fakhra. Iran imepata mafanikio hayo pamoja na kuwepo vikwazo vya kidhalimu vya madola ya Magharibi.

 

Tags