Feb 17, 2022 03:19 UTC
  • Iran yafanyia majaribio yaliyofana chanjo ya kukabiliana na Omicron

Shirika la Kutengeneza Dawa la Shifa la Iran limetangaza mafanikio makubwa ya awali katika majaribio ya chanjo ya kukabiliana na COVID-19 aina ya Omicron.

Kwa mujibu wa taarifa, majaribio yaliyofanyiwa chanjo hiyo kwa wanyama yameonyesha mafanikio ya asilimia 100 katika kukabilkiana na kirusi hicho.

Shirika la Kutengeneza Dawa la Shifa ambalo ndilo lililotengeneza chanjo maarufu ya Iran ya COVID-19 ijulikanayo kama COVIran Barekat limesema, lilianza utafiti wa kuzalisha chanjo mpya ya kukabiliana na Omicron punde baada ya aina hiyo ya COVID-19 kuripotiwa nchini Iran.

Shirika la Shifa limesema tayari limeanza kuzalisha kwa wingi chanjo hiyo ya kukabiliana na Omicron na limeshawasilisha maombi kwa Shirika la Dawa na Chakula Iran ili kupata idhini ya majaribio kwa mwanadamu.

Chanjo ya Iran ya Razi Cov Pars

Iran imtengenezea chanjo kadhaa za COVID-19 na baadhi ya chanjo hizo zimeanza kutumiwa. Chanjo hizo ni pamoja na COVIran Barekat, PastoCoVac, ambayo imeundwa kwa ushirikiano wa taasisi ya Pasteur ya Iran na Taasisi ya Finlay ya Cuba, na Razi Cov Pars iliyotengenezwa na Taasisi ya Utafiti wa Chanjo ya Razi. Chanjo hizo tayari zinatumika katika zoezi la chanjo nchini Iran.

 Chanjo nyingine ambayo imeanza kutumika hivi karibuni nchini Iran ni ile ya Spikogen ambayo imetengenezwa kwa ushirikiano baina ya shirika la CinnaGen la Iran na shirika la Vaxine la Australia. 

Chanjo hizo zinasubiri idhini ya Shirika la Afya Duniani kuanza kuuzwa katika soko la kimataifa. Chanjo zingine za Iran ambazo zingali zinafanyiwa majaribio ya mwisho ni Noora na Fakhra.

Tags