Shamkhani: Kuweko wanajeshi wa Marekani ndicho kikwazo cha kupatikana amani Syria
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uwepo wanajeshi vamizi wa Marekani nchini Syria ndicho kikwazo kikuu cha kupatikana amani katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Admiral Ali Shamkhani alisema hayo jana (Jumapili) wakati alipoonana na Meja Jenerali Ali Mamlouk, Mkuu wa Ofisi ya Usalama wa Taifa ya Syria aliyepo ziarani hapa Tehran.
Shamkhani amebainisha nafasi haribifu ya Marekani ya kuzusha migogoro katika eneo hili na duniani kiujumla kwa shabaha ya kufanikisha malengo yake ya kibeberu na kupora utajiri wa mataifa ya dunia na kuongeza kuwa, wanajeshi vamizi wa Marekani ndani ya ardhi ya Syria ndilo tatizo kubwa na ndio wanaokwamisha juhudi za kurejesha amani na utulivu nchini humo.
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, jinai za Marekani za kuyapa mafunzo ya kijeshi magenge ya kigaidi nchini Syria si tu kunakwamisha juhudi za kupatikana amani lakini pia ni tishio kwa usalama wa eneo hili zima.
Vile vile amegusia uhusiano mzuri uliopo baina ya Iran na Syria na kutilia mkazo wajibu wa kuharakishwa utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa na pande mbili hasa katika masuala ya kiuchumi.
Kwa upande wake Meja Jenerali Ali Mamlouk, Mkuu wa Ofisi ya Usalama wa Taifa ya Syria ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa uungaji mkono wake kwa wananchi wa Syria katika vita dhidi ya ugaidi na uafiriti wa Marekani na kutilia mkazo wajibu wa kuendelezwa ushirikiano wa nchi hizi mbili ndugu katika nyuga zote.