Usafirishaji wa bidhaa za Iran nchini Afrika Kusini waongezeka kwa asilimia 500
Mkuu wa Shirika la Ustawi wa Kibiashara la Iran limetangaza kuwa, usafirishaji nje bidhaa za Iran umepindukia dola bilioni 13 huku nchi za Afrika Kusini na Ghana zikiongoza kwa barani Afrika.
Alireza Peyman-Pak ametangaza habari hiyo na kutoa ufafanuzi kwa kusema, mwaka uliopita wa Kiirani wa 1400 Hijria Shamsia, Tehran imefanikiwa kusafirisha nje ya nchi bidhaa mbalimbali zenye thamani ya dola bilioni 13 kwa nchi za Afrika, Asia na barani Ulaya.
Amesema, usafirishaji wa bidhaa za Iran huko Indonesia umeongezeka kwa asilimia 70, katika nchi ya Kiafrika ya Ghana umeongezeka kwa asilimia 150 na asilimia 500 kwa Afrika Kusini.
Miongoni mwa mikakati mikuu ya serikali ya 13 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kupanua wigo wa usafirishaji nje bidhaa kwa nchi mbalimbali ulimwenguni.
Sasa hivi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejipanga vizuri pia kuongeza kiwango cha biashara zake na nchi yenye watu wengi ya China na imetabiriwa kuwa mabadilishano hayo yatafikia dola bilioni 100.
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Mkuu wa Shirika la Ustawi wa Kibiashara la Iran amesema, katika mwaka wa Kiirani wa 1400 Hijria Shamsia, usafirishaji nje wa bidhaa zisizo za mafuta za Iran ulifikia dola bilioni 48 ambapo kwa mwaka huo, iliingiza bidhaa zenye thamani ya dola bilini 53.
Peyman-Pak pia amegusia kuongezeka usafirishaji wa bidhaa za Iran kwa nchi jirani na kutoa ufafanuzi kwa kusema, kiwango hicho kiliongezeka kwa asilimia 65 kwa bidhaa za Iran zilizopelekwa nchini Oman na asilimia 140 kwa bidhaa hizo zilizopelekwa nchini Uturuki.