Raisi: Iran inapinga uingiliaji wowote wa ajinabi nchini Syria
(last modified Sun, 10 Jul 2022 09:09:18 GMT )
Jul 10, 2022 09:09 UTC
  • Raisi: Iran inapinga uingiliaji wowote wa ajinabi nchini Syria

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Iran inaunga mkono amani na uthabiti na inapinga uingiliaji wowote wa madola ajinabi katika mambo ya ndani ya Syria.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyasema hayo Jumamosi jioni alipompigia simu Rais Bashar al Asad wa Syria na kumpongeza yeye binafsi, serikali na watu wa Syria kwa mnasaba wa siku kuu ya Idul Adh'ha. Katika mazungumzo hayo, Rais Raisi amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kuunga mkono mhimili wa muqawama au mapambano hasa Syria na kuongeza kuwa: "Iran inaunga mkono uwepo wa amani na uthabiti na inapinga uingiliaji wowote wa ajinabi nchini Syria."

Kwa upande wake, Rais Bashar al Asad wa Syria ameipongeza serikali na watu wa Iran kwa mnasbaa wa kuwadia siku kuu ya Idul Adh'ha ambapo pia amemuomba Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amfikishie salamu maalumu za pongezi, kheri na fanaka Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Rais Asad wa Syria katika Sala ya Idul Adh'ha

Hali kadhalika rais wa Syria amesema maadui wanaendelea kudhoofika zaidi mbele ya mhimili wa muqawama na kuongeza kuwa, Iran na Syria zinalindana huku akibainisha matumaini yake kuwa, katika sherehe za idi miaka ijayo, mataifa ya Syria na Iran yatakuwa yamepata mafanikio makubwa kitaifa na kimataifa.

Wananchi wa Iran na nchi nyingine nyingi duniani leo wanaadhimisha sikukuu ya Idul Adh'ha sambamba na mahujaji wanaokamilisha ibada ya Hija huko Makka nchini Saudi Arabia. Jana pia ilikuwa siku kuu ya Idul Adh'ha katika baadhi ya maeneo duniani.

Tarehe 10 Dhulhija mahujaji waliokwenda Makka kwa ajili ya ibada ya Hija huchinja mnyama na kumtoa sadaka wakitekeleza amri ya Mwenyezi Mungu SW na kuhuisha kumbukumbu ya Nabii Ibrahim (as).