"Marekani ikiwa na irada ya kisiasa kama Iran, makubaliano yatafikiwa"
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu haitakubali kushinikizwa juu ya kufikia haraka muafaka wa kujaribu kuhuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Nasser Kan'ani Chafi amesema hayo leo hapa mjini Tehran katika kikao cha kila wiki na waandishi wa habari na kuongeza kuwa, iwapo Marekani ingelikuwa na irada ya kisiasa kama Iran, basi makubaliano yatafikiwa katika kipindi kifupi kijacho.
Amesisitiza kuwa, "Iran haichukui hatua kwa misingi ya jazba au pupa, na kamwe haiwezi kutoa muhanga maslahi ya taifa hili kwa kukubali kuburuzwa kwenye mchakato wa kuharakishwa."
Amesema Marekani imeanzisha vita vya kisaokolojia dhidi ya Iran, na kutaka kuonesha kuwa hakuna muda wa kuendelea kufanya mazungumzo, na kwa msingi huo sharti Iran isaini makubaliano hayo haraka iwezekanavyo.
Kan'ani amesema Marekani inapaswa kukubali masharti yote ya Iran kwa mujibu wa mapatano hayo ya kimataifa ya mwaka 2015, na kusisitiza kwamba kurefusha mazungumzo ya kujaribu kuhuisha makubaliano hayo hakuna maslahi kwa upande wowote hususan Wamarekani.
Kuhusu vita vya Ukraine, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Tehran haiungi mkono chaguo lolote la kijeshi kwa ajili ya kutatua mizozo ya kieneo, na kwamba chaguo bora la (kumaliza vita vya) Ukraine ni ufumbuzi wa kisiasa.
Amekosoa upotoshaji wa vyombo vya habari vya Magharibi kufuatia safari ya Rais Vladimir Putin wa Russia hapa nchini na kueleza bayana kuwa: Tuna imani na suluhisho la kisiasa, na wala hatusimami upande mmoja dhidi ya upande wa pili.