Iran inakaribisha njia ya diplomasia na mazungumzo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i86364-iran_inakaribisha_njia_ya_diplomasia_na_mazungumzo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anasema Tehran inakaribisha kuendelea njia ya diplomasia kwa madhumuni ya kufikia makubaliano juu ya kuondolewa vikwazo dhidi yake na kuhuisha mapatano ya nyuklia ya  2015, huku akihimiza Marekani izingatie uhalisia wa mambo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 28, 2022 03:27 UTC
  • Iran inakaribisha njia ya diplomasia na mazungumzo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anasema Tehran inakaribisha kuendelea njia ya diplomasia kwa madhumuni ya kufikia makubaliano juu ya kuondolewa vikwazo dhidi yake na kuhuisha mapatano ya nyuklia ya  2015, huku akihimiza Marekani izingatie uhalisia wa mambo.

Katika mazungumzo ya simu na Mkuu wa Sera ya Mambo ya Nje ya Umoja wa Ulaya (EU) Josep Borrell Jumatano, Hossein Amir-Abdollahian alizungumzia suala la mpango wa hivi karibuni wa umoja huo, akisema kwamba Iran "inakaribisha mwendelezo wa njia ya diplomasia na mazungumzo" kufikia mapatano.

Borrell Jumanne alisema alikuwa amependekeza rasimu mapya ya kuhusia mapatano  ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utendaji (JCPOA).

"Rasimu hiyo inawakilisha mapatano bora zaidi ambayo mimi, kama mwezeshaji wa mazungumzo, naona kama inayowezekana. Sio makubaliano bora zaidi,  lakini yanashughulikia mambo yote muhimu,” ameandika katika nakala ya Jarida la Financial Times.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amemwambia mwenzake wa Ulaya kwamba Marekani inasema kila wakati inataka makubaliano, na kuongeza kuwa ikiwa madai hayo ni ya kweli basi hilo linapaswa kuonekana katika maandishi ya makubaliano na kivitendo.

"Hakuna shaka juu ya azma ya serikali ya Jamhuri ya Kiislamu kuhusu kufikia makubaliano mazuri, yenye nguvu, na endelevu," Amir-Abdollahian amesema huku akimshukuru Borrell na naibu wake Enrique Mora kwa juhudi zao za kufikia makubaliano.

Borrell, kwa upande wake, amesema upande wa Iran umeonyesha utashi wake mzuri na wenye uzito wakati wa mazungumzo, na kuongeza kuwa ni wakati wa mazungumzo kutoa matokeo.

Afisa wa juu wa sera ya kigeni katika Umoja wa Ulaya amesisitiza juu ya utayari wake na naibu wake kusaidia kuwezesha na kuharakisha mchakato huu kupitia mashauriano na pande zote husika.

Marekani ilirudisha vikwazo dhidi ya Iran mnamo Mei 2018 baada ya kujitondoa katika makubaliano ya kihistoria ya JCPOA kati ya madola sita makubwa dunaini na Iran yaliyofikiwa mnamo 2015.

Mji mkuu wa Austria wa Vienna umekuwa mwenyeji wa raundi kadhaa za mazungumzo tangu Aprili mwaka jana kati ya Iran na nchi zilizobaki katika maptano ya JCPOA ambayo yamekuwa yakifanyika kuchunguza kuondolewa kwa vikwazo na kuhuisha mapatano hayo.

Mazungumzo yalihamishwa kwenda mji mkuu wa Qatari mapema mwaka huu, na Umoja wa Ulaya umepewa jukumu la kuratibu mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani. Mazungumzo ya kwanza Doha yalifanyika mwezi uliopita lakini Marekani ilionekana kushindwa kuchukua maamuzi.

Amir-Abdollahian amesema ikiwa Marekani itachukua hatua kwa kuzingatia uhalisia wa mambo basi makubaliano mazuri yatapatikana.

Amebaini kuwa Jamhuri ya Kiislamu tangu mwanzo wa mazungumzo imeonyesha nia yake nzuri na dhamira kubwa kuelekea kufikia makubaliano.