Kani: Iran iko tayari kuipa Marekani fursa nyingine ya kujirudi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i86492-kani_iran_iko_tayari_kuipa_marekani_fursa_nyingine_ya_kujirudi
Kiongozi wa timu ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia ya Vienna amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ipo tayari kutamatisha mazungumzo ya kuiondolea vikwazo Tehran haraka iwezekanavyo, sanjari na kuipa Marekani fursa nyingine ya kurekebisha makosa yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 31, 2022 22:17 UTC
  • Kani: Iran iko tayari kuipa Marekani fursa nyingine ya kujirudi

Kiongozi wa timu ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia ya Vienna amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ipo tayari kutamatisha mazungumzo ya kuiondolea vikwazo Tehran haraka iwezekanavyo, sanjari na kuipa Marekani fursa nyingine ya kurekebisha makosa yake.

Ali Bagheri Kani alisema hayo jana Jumapili kwenye mtandao wa Twitter na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ipo tayari kuhakikisha kuwa mazungumzo hayo yanamalizika haraka iwapo upande wa upili utaonyesha utayarifu wake.

Ameeleza kuwa, "Iran inafanya kazi kwa karibu na washiriki wengine wa JCPOA, hususan Mratibu, ili kuipa Marekani fursa nyingine ya kuonesha nia njema na kuwa na uwajibikaji."

Ali Bagheri Kani ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya kisiasa ameiasa Marekani kutilia maanani uhalisia wa mambo na kujiepusha na tabia ya kupenda makuu ili mazungumzo yafikie kikomo ndani ya muda mfupi ujao.

Kikao cha Vienna, Austria

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza bayana kuwa, mienendo ya kiuwajibikaji ya upande wa Magharibi ndio sharti la kufikiwa makubaliano ya mwisho katika mazungumzo ya Vienna.

Mazungumzo ya Vienna ya kuiondolea vikwazo haramu taifa la Iran yamesita kwa karibu miezi minne, baada ya kufanyika duru kadhaa kati ya Iran na kundi la 4+1.